Na Mwandishi Wetu
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imesema imejipanga kutumia Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) kutoa elimu kwa wananchi kuhusu haki za binadamu na utawala bora pamoja na huduma mbalimbali zinazotolewa na tume hiyo.
Akizungumza katika banda la Tume hiyo kwenye maonesho hayo, Mkurugenzi wa Sheria wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Ellen Ruyage, alisema wananchi wanaotembelea banda hilo wanapata fursa ya kufahamu majukumu ya tume, kuwasilisha malalamiko yanayohusu ukiukwaji wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora, pamoja na kupata ushauri na msaada wa kisheria.
Alisema tume inapokea malalamiko yote yanayohusu uvunjifu wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora, kisha kuyafanyia kazi kwa mujibu wa sheria, huku ikitoa maelezo kwa walalamikaji kuhusu hatua zinazochukuliwa.
"Tunapokea malalamiko yote yanayohusiana na uvunjifu wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.
Aidha, tunatoa huduma za msaada wa kisheria pamoja na elimu kuhusu haki za binadamu na utawala bora ili wananchi wajue haki zao na namna ya kuzidai," alisema Ruyage.
Alifafanua kuwa si kila mwananchi anayewasilisha malalamiko yake hukumbana na ukiukwaji wa haki za binadamu au misingi ya utawala bora, bali wakati mwingine tatizo linaweza kuwa nje ya mamlaka ya tume. Hata hivyo, alisema tume huwapa mwongozo wa mahali sahihi pa kupata huduma ili kuhakikisha haki zao hazicheleweshwi.
Ruyage alisema juhudi za tume za kuendelea kutoa elimu zimeongeza uelewa wa wananchi, hali inayowafanya kujitokeza kwa wingi kuripoti matukio ya ukiukwaji wa haki zao na pale wanapoona misingi ya utawala bora haifuatwi.
Aliongeza kuwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi, ikiwemo mashirika ya kimataifa, hatua ambayo imewezesha huduma zake kuwafikia wananchi wengi zaidi katika maeneo mbalimbali nchini.
Aidha, alitoa wito kwa wananchi kutumia fursa ya maonesho ya Sabasaba kutembelea banda la tume ili kupata elimu, ushauri wa kisheria na kuwasilisha changamoto zozote zinazohusu haki za binadamu na utawala bora.
"Tume yetu iko wazi kwa wananchi wote. Tunawahimiza wajitokeze kupata huduma na elimu ili kujenga jamii inayozingatia haki za binadamu na misingi ya utawala bora," alisisitiza





Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...