Vijana wa Tanzania wametakiwa kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta ya bahari, huku Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) kikieleza kuwa wahitimu wake wanaendelea kupata ajira ndani na nje ya nchi, hususan katika mataifa ya Mashariki ya Kati kutokana na mahitaji makubwa ya wataalamu wa ubaharia.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) Julai 13, 2026, Nahodha na Mwalimu kwa Njia ya Vitendo Daraja la Pili wa DMI, Master Kelly Mwandambo, amesema ubaharia ni taaluma yenye fursa nyingi za ajira na kipato kizuri, hivyo vijana wanapaswa kuichagua kama taaluma ya ndoto zao.

Amesema bado jamii imekuwa na dhana potofu kuwa ubaharia ni fani ya wanaume au watu wahuni, jambo ambalo si la kweli, akisisitiza kuwa taaluma hiyo ni ya kitaaluma kama zilivyo taaluma nyingine na wanawake wana nafasi sawa ya kufanikiwa.

Mwandambo amesema mafunzo ya ubaharia yanafuata viwango vya kimataifa vinavyosimamiwa na Shirika la Kimataifa la Bahari, hali inayowafanya wahitimu wa DMI kuwa na uwezo wa kushindana katika soko la ajira duniani kwa kuwa wanapata mafunzo yanayolingana na yanayotolewa katika nchi nyingine ikiwemo Marekani.

Aidha, amewataka wazazi na walezi kuwahamasisha watoto wao kujiunga na Chuo cha Bahari Dar es Salaam, akieleza kuwa taasisi hiyo inatoa mafunzo kuanzia ngazi ya cheti hadi Shahada za Uzamili (Masters), hatua inayowafungulia wahitimu fursa za ajira katika sekta ya bahari duniani.

Kwa upande wake, Mkufunzi Msaidizi wa DMI na Mhandisi wa Baharini, Winfrida Winsislaus Ngalu, amesema wanafunzi wanaojiunga na chuo hicho wanapata fursa mbalimbali za ufadhili wa masomo, ikiwemo mikopo ya serikali kuanzia ngazi ya cheti, Samia Scholarship, mikopo ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na MELT Fund kwa wanaosoma kozi zinazohusiana na ubaharia.

Amesema pamoja na ufadhili huo, wahitimu wa DMI wameendelea kuwa miongoni mwa wataalamu wanaohitajika zaidi katika soko la ajira la kimataifa, jambo linaloifanya sekta ya bahari kuwa moja ya maeneo yenye mustakabali mzuri kwa vijana wanaotafuta taaluma yenye ajira za uhakika na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa Taifa. 








Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...