Na Mwandishi Wetu
NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Ayoub Mohammed, amesema Zanzibar ina uwezo mkubwa wa kuimarisha uchumi kupitia biashara, utalii na utamaduni, huku akisisitiza umuhimu wa kuzalisha bidhaa na huduma zenye ubora wa kushindana katika masoko ya ndani na kimataifa.

Akizungumza alipokuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Zanzibar ndani ya Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Ayoub alisema licha ya ukubwa mdogo wa kijiografia wa Zanzibar, visiwa hivyo vina historia, fursa na uwezo mkubwa wa kuwa kitovu cha biashara na uwekezaji.

"Tukiri kwamba kwa ukubwa wa eneo Zanzibar ni ndogo, lakini kwa ubora wa bidhaa na huduma Zanzibar ni kubwa zaidi ya tunavyofikiria. Tuende tukashindane kwa ubora wa bidhaa, ubora wa vifungashio na ubora wa utoaji wa huduma," alisema.

Alieleza kuwa historia ya Zanzibar kama lango la biashara katika Bahari ya Hindi inapaswa kuendelea kutumika kuvutia wawekezaji na kufungua masoko mapya ya bidhaa na huduma zinazozalishwa visiwani.

Ayoub alisema maadhimisho ya miaka 50 ya Sabasaba yameendelea kudhihirisha mchango wa maonesho hayo katika kukuza biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi, huku Zanzibar ikinufaika kwa kutangaza bidhaa zake na ubunifu wa wananchi.

Aidha, alisema utamaduni wa Zanzibar ni rasilimali muhimu ya kiuchumi inayoweza kuongeza mapato kupitia sekta za utalii, sanaa na biashara. Alisisitiza umuhimu wa kuendeleza mavazi ya asili, muziki wa taarabu na mila mbalimbali kama vivutio vinavyoweza kuongeza thamani ya utalii wa Zanzibar.

Pia alihimiza kuendelea kukuza matumizi ya Kiswahili kama nyenzo ya biashara na utalii, akisema lugha hiyo imeendelea kufungua fursa za ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi ndani na nje ya nchi.

Katika hotuba yake, Ayoub alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake, akisema umeendelea kudumisha amani na usalama nchini, hali inayoweka mazingira wezeshi kwa biashara, uwekezaji na maendeleo.

Aliwataka wafanyabiashara na wawekezaji kutumia fursa zilizopo Zanzibar kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na kuwekeza katika sekta mbalimbali kwa lengo la kukuza uchumi endelevu na kuongeza ustawi wa wananchi.
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...