Na Janeth Raphael - MichuziTv

Watendaji wa Serikali za Mitaa nchini wamehimizwa kutenganisha majukumu yao ya kiutumishi na shughuli za kisiasa ili kulinda weledi, uadilifu na kutenda haki kwa wananchi, hatua itakayosaidia kuimarisha imani ya umma kwa Serikali pamoja na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma.

Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Watendaji wa Serikali za Mitaa Tanzania (UWATA), Frank Kalinga, wakati wa uzinduzi rasmi wa umoja huo uliofanyika jijini Dodoma.

Kalinga amesema hadhi na heshima ya watendaji wa Serikali za Mitaa inategemea namna wanavyotekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya utumishi wa umma, huku wakiepuka kuchanganya wajibu wao wa kitaaluma na shughuli za kisiasa.

Amesisitiza kuwa watendaji ni kiungo muhimu kati ya Serikali na wananchi katika ngazi za msingi, hivyo wanapaswa kujenga mazingira ya kuaminika kupitia utendaji wenye uwazi, uwajibikaji na usio na upendeleo.

"Ni muhimu kila mdau kuheshimu mipaka ya mamlaka na majukumu yaliyoainishwa kisheria ili kuimarisha uwajibikaji na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi," amesema Kalinga.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Sospeter Mtwale, amesema kuanzishwa kwa UWATA ni hatua muhimu itakayosaidia kuimarisha uwezo wa watendaji wa Serikali za Mitaa, kukuza maadili ya utumishi wa umma na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa sera pamoja na miradi ya maendeleo katika ngazi za kata, vijiji na mitaa.

Mtwale amewataka watendaji kuendelea kuzingatia misingi ya utawala bora, uzalendo, uwajibikaji na usimamizi makini wa rasilimali za umma ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.

Ameeleza kuwa watendaji wana nafasi ya kipekee katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kwamba usimamizi madhubuti wa miradi ya maendeleo utachangia kuleta matokeo chanya, kuongeza thamani ya fedha za umma na kuharakisha maendeleo katika jamii.










Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...