Na Janeth Raphael - MichuziTv

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali itaendelea kuimarisha maridhiano ya kisiasa kama msingi wa kuendeleza mchakato wa maboresho ya Katiba, huku akisisitiza kuwa hatua zote zitafanyika kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi kwa maslahi mapana ya Taifa.

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Julai 30, 2026, alipokutana na viongozi wa vyama 18 vya siasa nchini katika Ikulu ya Dar es Salaam, kwenye mkutano uliolenga kujadili masuala ya maridhiano ya kisiasa, mageuzi ya kisiasa, uchumi, huduma za jamii, ajira, uwekezaji na ulinzi wa amani nchini.

Akizungumza katika mkutano huo, Rais Samia alisema Serikali imejipanga kuendelea kushirikiana na vyama vya siasa ili kuhakikisha mchakato wa maridhiano unazaa matokeo yenye manufaa kwa Taifa, ikiwa ni pamoja na kufungua njia kuelekea hatua zinazofuata za maboresho ya Katiba.

Aidha, amewafahamisha viongozi hao kuhusu hatua zilizofikiwa katika maandalizi ya mchakato wa maridhiano visiwani Zanzibar, akieleza kuwa Serikali itaendelea kusimamia mchakato huo kwa uwazi na kwa kuzingatia misingi ya kisheria.

Rais Samia pia alitangaza kuwa Serikali itaendelea kufanya mikutano ya mazungumzo na viongozi wa vyama vya siasa angalau mara tatu kwa mwaka, akisema hatua hiyo inalenga kuimarisha ushirikiano, kujenga uelewano na kutatua changamoto mbalimbali kupitia majadiliano.

Mbali na masuala ya kisiasa, Rais Samia alielezea hali ya uchumi wa nchi, akisema Tanzania imeendelea kushuhudia ukuaji wa uchumi wa asilimia sita katika mwaka uliopita, huku ukuaji wa asilimia 6.3 ukitarajiwa kufikiwa mwaka huu.

Amesema Serikali inaendelea kuweka mkazo katika kukamilisha miradi mikubwa ya maendeleo iliyoanza kutekelezwa pamoja na kuwekeza zaidi katika miundombinu ya kimkakati, ikiwemo reli, barabara, bandari na sekta nyingine muhimu kwa maendeleo ya uchumi.

Kuhusu uwekezaji, Rais Samia alisema maboresho yaliyofanyika katika Bandari ya Dar es Salaam yameongeza uwezo wa bandari hiyo kuhudumia biashara ya ndani na kikanda, huku Serikali ikiendelea kupanua na kuboresha shughuli za bandari za Bahari ya Hindi pamoja na zile za maziwa ya Victoria, Tanganyika na Nyasa.

Aidha, amewataka viongozi wa vyama vya siasa kushirikiana katika kulinda amani, umoja na maslahi ya Taifa, akisisitiza kuwa ulinzi wa Tanzania ni jukumu la pamoja linalohusisha Serikali, vyama vya siasa na wananchi wote.

Katika mkutano huo, viongozi wa vyama vya siasa waliwasilisha maoni na mapendekezo yao kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya kisiasa, kijamii na kiuchumi. Serikali iliahidi kuendelea kuyapokea na kuyafanyia kazi kupitia majukwaa rasmi ya majadiliano na mifumo ya maamuzi.

Mkutano huo ni wa pili kuitishwa na Rais Samia tangu kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Mkutano wa kwanza ulifanyika Machi 31, 2026, Ikulu ya Dar es Salaam, ukiwakutanisha wagombea wa urais na wagombea wenza kutoka vyama vya siasa vilivyoshiriki uchaguzi huo.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...