NA DENIS MLOWE, IRINGA


WAKALA Mkuu wa mbegu za Taasisi ya ASA mkoani Iringa, Kampuni ya Mgongolwa Agrovet & Seeds Company Limited, imewahimiza wakulima kutumia mbegu bora zinazozalishwa na Taasisi ya ASA ili kuongeza uzalishaji wa mazao na kuondokana na changamoto ya kutumia mbegu zisizo na ubora.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Iringa Press Club, Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Joseph Saidi Mgongolwa, alisema wamepewa dhamana na Taasisi ya ASA iliyo chini ya Wizara ya Kilimo kuhakikisha mbegu bora zinawafikia wakulima wa vijijini na mijini kwa wakati kabla ya kuanza kwa msimu wa kilimo.

Alisema hatua hiyo ni sehemu ya maandalizi kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wakulima (Nanenane), huku lengo likiwa kuwafikishia wakulima mbegu zenye ubora wa hali ya juu kwa bei nafuu ili kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao.

Mgongolwa alisema Taasisi ya ASA imeamua kusogeza huduma karibu na wakulima kupitia mawakala wake ili kuhakikisha kila mkulima, mdogo na mkubwa, anapata mbegu bora zinazokidhi mahitaji ya maeneo mbalimbali ya kilimo nchini.
Alieleza kuwa kampuni hiyo itasambaza mbegu za mahindi zinazofaa kwa maeneo yenye mvua chache na maeneo yenye mvua nyingi, pamoja na mbegu za mpunga, alizeti na maharage ya njano na mekundu.

"Tunawaomba wakulima wa mkoa wa Iringa na Watanzania kwa ujumla kuamini mbegu za ASA ambazo zinazalishwa chini ya Wizara ya Kilimo. Mbegu hizi zimeonyesha uwezo mkubwa wa kuongeza mavuno na zinapatikana kwa bei nafuu ili kumwezesha mkulima kupata tija zaidi," alisema.

Aidha alisema kampuni hiyo imejipanga kufungua vituo vya usambazaji katika maeneo mbalimbali ya vijijini ili kurahisisha upatikanaji wa mbegu hizo, huku duka kuu likiwa katika eneo la CCM Mkoa wa Iringa.

Mgongolwa alisema moja ya changamoto kubwa iliyokuwa ikiwakabili wakulima ni uwepo wa mbegu feki, hali iliyosababisha wengi kupata hasara kutokana na mavuno hafifu.

Alisema kampuni yake itahakikisha mbegu zote zinazosambazwa ni halisi kutoka Taasisi ya ASA na zitakuwa na alama maalumu za utambuzi ikiwemo nembo ya Taifa ili kuondoa uwezekano wa wakulima kununua mbegu bandia.

"Nami ni mkulima na nimewahi kutumia mbegu mbalimbali baada ya kutumia mbegu za ASA nilishuhudia ongezeko kubwa la mavuno, ndiyo maana ninawahamasisha wakulima wenzangu kuzitumia kwa maendeleo ya kilimo chetu," alisema.

Kwa upande wa sifa za baadhi ya mbegu, alisema mbegu ya mahindi aina ya T105 hustawi katika maeneo yenye urefu wa mita 800 hadi 1,500 kutoka usawa wa bahari, hukomaa ndani ya siku 105 hadi 115 na inaweza kutoa magunia 18 hadi 22 kwa ekari endapo mkulima atazingatia kanuni bora za kilimo.

Aliongeza kuwa mbegu ya mpunga aina ya TXD 306 (Saro 5) imekusudiwa kwa maeneo ya mabondeni na skimu za umwagiliaji, hukomaa ndani ya siku 110 hadi 120, huku ikiwa na sifa ya kutoa mchele usiovunjika kirahisi wakati wa kukobolewa na wenye harufu nzuri.

Kwa mbegu ya alizeti aina ya Record, alisema hustawi katika maeneo yenye urefu wa mita 0 hadi 2,400 kutoka usawa wa bahari, hukomaa ndani ya siku 110 hadi 120 na inaweza kutoa mavuno ya kilo 600 hadi 800 kwa ekari, ikiwa na kiwango cha mafuta kati ya asilimia 32 na 48.

Mgongolwa alitoa wito kwa wakulima kutumia mbegu bora zilizoidhinishwa na serikali ili kuongeza uzalishaji wa mazao, kuimarisha usalama wa chakula na kuongeza kipato cha kaya kupitia kilimo chenye tija.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...