Na Janeth Raphael - MichuziTv 

Mfumo wa Stakabadhi za Ghala umeendelea kuonyesha mafanikio makubwa nchini baada ya kuwawezesha wakulima na wazalishaji kuingiza zaidi ya Shilingi trilioni 2.2 kupitia mauzo ya mazao katika mwaka wa fedha 2025/2026, huku kiasi cha mazao yaliyouzwa kupitia mfumo huo kikiongezeka kwa asilimia 43.6 ikilinganishwa na mwaka uliopita.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) kwa mwaka wa fedha 2025/2026 na mwelekeo wa mwaka wa fedha 2026/2027, Mkurugenzi Mtendaji wa WRRB,  Asangye Bangu, amesema mafanikio hayo yanaakisi kuongezeka kwa imani ya wakulima na wadau katika matumizi ya mfumo huo.

Amesema Mfumo wa Stakabadhi za Ghala ulianza kutekelezwa kwa zao la korosho pekee, lakini kwa sasa umejumuisha mazao na bidhaa 18, ikiwemo kahawa, kakao, ufuta, soya, mbaazi, dengu, choroko, mahindi, mpunga, mchele, chai, maharage, karanga, asali, mihogo na vitunguu swaumu. Aidha, mfumo huo sasa unatekelezwa katika mikoa 23 nchini, hatua inayoonesha kupanuka kwa wigo wa huduma na kuimarika kwa masoko ya mazao.

 Bangu amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026 Serikali ilitoa Shilingi milioni 950 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya WRRB. Fedha hizo zilielekezwa katika utoaji wa elimu na uhamasishaji kwa wakulima na wadau, uboreshaji wa miundombinu ya TEHAMA na mifumo ya kidijitali, kuimarisha ukaguzi na usimamizi wa maghala pamoja na ununuzi wa vitendea kazi vilivyoongeza ufanisi wa taasisi hiyo.

Ameeleza kuwa uwekezaji huo umeimarisha uwezo wa WRRB kusimamia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala kwa ufanisi zaidi na kuongeza upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi.

Akifafanua mafanikio ya mfumo huo, amesema jumla ya kilo 1,122,246,475 za mazao tisa ambayo ni korosho, ufuta, kahawa, kakao, mbaazi, dengu, choroko, soya na chai ziliuzwa kupitia minada ya kidijitali inayosimamiwa na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), ikilinganishwa na kilo 781,659,285 zilizouzwa mwaka uliotangulia.

"Ongezeko hili la zaidi ya kilo milioni 340 ndani ya mwaka mmoja linaonesha kuwa wakulima wengi zaidi wanaendelea kuuamini Mfumo wa Stakabadhi za Ghala kutokana na uwazi, ushindani wa bei na uhakika wa soko unaopatikana kupitia mfumo huu," amesema.

Kutokana na mauzo hayo, wakulima na wauzaji walilipwa jumla ya Shilingi trilioni 2.298, huku Serikali za Mitaa zikikusanya Shilingi bilioni 61.05 kupitia ushuru wa mazao (CESS). Aidha, thamani ya biashara yote iliyofanyika kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala ilifikia Shilingi trilioni 2.679.

 Bangu amesema fedha zilizowafikia wakulima zimechangia kuinua uchumi wa kaya kwa kuwawezesha kumudu gharama za elimu, afya, makazi na kuongeza uwekezaji katika shughuli za uzalishaji.

Aidha, amesema mapato yaliyopatikana kupitia ushuru wa mazao yameziwezesha Halmashauri kuimarisha utoaji wa huduma za jamii kwa kuwekeza katika ujenzi na ukarabati wa barabara, shule, vituo vya afya, masoko na miundombinu mingine muhimu inayowanufaisha wananchi.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...