Jane Mwakyoma - Rukwa.
WAKAZI wa kata ya Msua Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa wameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa ujenzi wa shule ya msingi Kisiwani inayowasaidia wanafunzi wa eneo hilo kupata elimu karibu na makazi yao.
Wakizungumza baada ya waziri wa katiba na sheria Juma Homera kutembelea na kukagua ujenzi unaoendelea shuleni hapo wananchi wamesema ujenzi wa shule hiyo unasaidia watoto kupata elimu karibu na makazi yao ukilinganisha na hapo awali walikuwa wakifuata elimu hiyo zaidi ya km 3 hali iliyokuwa ikihatarisha usalama wa watoto hao.
Akimwakilisha mwalim mkuu wa shule ya msingi Kisiwani Efrahim Kimario amesema walipokea fedha za ujenzi zaidi ya Milioni 329 ikiwa majengo sita yamekamilika na tayari yanatumika huku jengo la utawala likiwa katika hatua ya umaliziaji kuhakikisha watoto wa eneo hilo wanaendelea kupata elimu ya msingi shuleni hapo.
Aidha amesema ujenzi wa shule hiyo unatumia mfumo wa Force Account ambapo alimshukuru Mbunge wa jimbo la Sumbawanga mjini Aishi Khalfan Hilali na Dtk. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada walizofanya kuhakikisha shule inajengwa na watoto wanapata elimu ya uhakika.
Kwa upande wake Waziri wa katiba na sheria Juma Homera amepongeza halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga kwa usimamizi wa mradi na kuhakikisha baadhi ya majengo yanakamilika na kuendelea kutoa huduma kwa wanafunzi.
Pia Homera amewataka viongozi wa serikali nchini kusimamia kikamilifu miradi ya maendeleo na kuhakikisha inakamilika kwa wakati ili kuepusha migogoro ya wananchi na serikali.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...