Na Mwandishi Wetu

WANANCHI kutoka maeneo mbalimbali nchini wameendelea kujitokeza kwa wingi kutembelea banda la Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, kwa lengo la kupata elimu kuhusu usalama, ubora na matumizi sahihi ya dawa, vifaa tiba na bidhaa nyingine za afya.

Katika banda hilo, wataalamu wa TMDA wamekuwa wakitoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kutambua dawa zilizosajiliwa na mamlaka hiyo, matumizi sahihi ya dawa, pamoja na umuhimu wa kununua dawa na bidhaa nyingine za afya kutoka kwenye maduka na vituo vilivyoidhinishwa ili kujikinga na bidhaa bandia au zisizo na ubora.

Aidha, wananchi wamepata fursa ya kuelezwa majukumu ya TMDA katika kusimamia ubora, usalama na ufanisi wa dawa, vifaa tiba na bidhaa nyingine za afya, sambamba na hatua zinazochukuliwa dhidi ya wanaojihusisha na usambazaji wa bidhaa zisizokidhi viwango.

Baadhi ya wananchi waliotembelea banda hilo wamesema elimu wanayoipata imewasaidia kuongeza uelewa kuhusu matumizi salama ya dawa na umuhimu wa kuhakiki bidhaa za afya kabla ya kuzitumia.

Wamesema maonesho hayo yamekuwa jukwaa muhimu la kuwafikia wataalamu wa TMDA na kupata majibu ya maswali mbalimbali yanayohusu matumizi ya dawa na bidhaa za afya, jambo linalochangia kuimarisha ulinzi wa afya za wananchi.

Kutokana na mwitikio huo, wananchi wamewahimiza Watanzania wengine kutumia fursa ya Maonesho ya Sabasaba kutembelea banda la TMDA ili kupata elimu itakayowasaidia kufanya maamuzi sahihi kuhusu matumizi ya dawa na bidhaa nyingine za afya, hatua ambayo itachangia kujenga jamii yenye afya na kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na matumizi ya bidhaa zisizo salama.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...