Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Yas Tanzania kwa kushirikiana na ZTE imezindua mpango maalumu wa kuwawezesha Watanzania kumiliki rauta za intaneti ya 5G kwa mfumo wa malipo ya awamu, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa huduma ya intaneti ya kasi kwa wafanyabiashara, kaya na taasisi mbalimbali nchini.
Mpango huo ulizinduliwa katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), ambapo wateja watapata fursa ya kumiliki rauta ya ZTE 5G kwa kulipa kiasi cha awali cha Sh80,000 na kisha Sh80,000 kila mwezi kwa kipindi cha miezi 12. Kila malipo ya mwezi yataambatana na kifurushi cha intaneti isiyo na kikomo chenye kasi ya Mbps 10.
Uzinduzi huo unakuja wakati Tanzania ikiendelea kushuhudia ukuaji wa uchumi wa kidijitali, huku matumizi ya malipo ya kidijitali yakiongezeka, huduma nyingi za Serikali zikihamia mtandaoni na mahitaji ya intaneti ya uhakika kwa ajili ya elimu, biashara na kazi yakiendelea kuongezeka.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Meneja wa Mauzo ya Vifaa vya Intaneti wa Yas Tanzania, Imelda Edward, alisema ushirikiano huo unalenga kuondoa kikwazo cha gharama ambacho kwa muda mrefu kimewazuia Watanzania wengi kupata huduma bora za intaneti.
Alisema intaneti ya uhakika si huduma ya mawasiliano pekee, bali ni nyenzo muhimu inayofungua fursa za kiuchumi na kijamii kwa wananchi.
"Leo mawasiliano si suala la kuunganishwa na intaneti pekee, bali ni kufungua fursa. Intaneti ya uhakika inawawezesha wajasiriamali kukuza biashara zao, wanafunzi kupata elimu ya kidijitali, wataalamu kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na familia kuendelea kuwasiliana. Kupitia ushirikiano wetu na ZTE tunafanya teknolojia ya kizazi kipya ipatikane kwa Watanzania wengi zaidi huku tukichochea ujumuishaji wa huduma za kidijitali nchini," alisema Imelda.
Aliongeza kuwa kwa wafanyabiashara wengi, intaneti imekuwa huduma muhimu kama ilivyo umeme, kwa kuwa ndiyo msingi wa malipo ya kidijitali, biashara mtandaoni, huduma kwa wateja na uendeshaji wa shughuli za kila siku.
"Kila oda inayofanyika mtandaoni, kila malipo ya kidijitali na kila mawasiliano na mteja yanategemea intaneti ya uhakika. Kupitia ushirikiano huu tunawapatia wafanyabiashara suluhisho za kidijitali zitakazowawezesha kuongeza ushindani, ubunifu na kukuza biashara zao," alisisitiza.
Kwa upande wake, mwakilishi wa ZTE, Wen Jiahao, alisema ushirikiano huo unaonesha dhamira ya kampuni hizo mbili ya kupanua upatikanaji wa teknolojia za kisasa za mawasiliano kwa gharama nafuu nchini.
Alisema kwa kuunganisha teknolojia ya 5G ya ZTE na mtandao mpana wa Yas Tanzania, wananchi, familia na wafanyabiashara watanufaika na huduma ya intaneti yenye kasi na uhakika zaidi, hivyo kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali unaokua kwa kasi.
Ushirikiano huo pia unaonesha dhamira ya Yas Tanzania ya kuendelea kuwekeza katika kuimarisha miundombinu ya kidijitali kupitia upanuzi wa mtandao wa 4G na 5G pamoja na kuanzisha suluhisho mbalimbali zitakazowaunganisha Watanzania wengi zaidi na fursa za uchumi wa kidijitali.
Katika Maonesho ya Sabasaba mwaka huu, wananchi wanaotembelea banda la Yas watapata fursa ya kujionea uwezo wa rauta ya ZTE 5G, kupata maelezo kuhusu mfumo wa malipo wa kuimiliki, huku kifaa hicho kikitarajiwa kupatikana katika maduka yote ya Yas nchini.
Mpango huo unatarajiwa kuchangia utekelezaji wa ajenda ya Taifa ya mageuzi ya kidijitali kwa kuongeza upatikanaji wa intaneti ya kasi kwa gharama nafuu, kuimarisha shughuli za biashara, kuongeza tija katika uchumi na kuwapa Watanzania wengi zaidi fursa ya kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...