Na Mwandishi Wetu,Kahama
WCHIMBAJI wadogo wa Dhahabu katikà kijiji cha Bukooba, Manispaa ya Kahama, mkoa wa Shinyanga, wameiomba Serikali kupelekewa huduma ya umeme na maji ili kurahisisha shughuli zao.
Wachimbaji hao wametoa maombi hayo mbele ya waandishi wa vyombo mbalimbali waliokwenda katikà mgodi huo kwa lengo la kujionea shughuli za uchimbaji Madini.
"Kwenye mgodi wetu huu wa Bukooba tunazo changamoto mbili kubwa. Kwanza hatuna umeme wa kuendeshea mitambo yetu ya uchimbaji na uchenjuaji, badala yake tunatumia dizeli na petroli hali ambayo inatuongezea gharama za uzalishaji ikizingatiwa Hali ya sasa ya bei za mafuta ambayo ipo juu", alieleza Mkurugenzi Mkuu wa mgodi huo Said Ibrahim Kapesya.
Aliongeza kuwa, "Pia tunayo changamoto nyingine ya ukosefu wa maji kwenye mgodi wetu kwa ajili ya kuchenjulia dhahabu. Hali hii inatusababishia usumbufu na gharama kubwa za uzalishaji kwasababu tunafuata maji umbali mrefu kutoka hapa, tunaiomba serikali ya mama yetu Rais Samia Suluhu Hassan itusogezee huduma hizi muhimu ili kurahisisha na kuboresha shughuli zetu", alibainisha Kapesya.
Kapesya aliishukuru serikali kwa kuwapatia leseni ya utafiti na uchimbaji katikà kijiji cha Bukooba bila kujali hali zao za kiuchumi, huku akimuomba waziri wa madini kutokimbilia kufuta leseni za wachimbaji wenye uwezo mdogo wa fedha bali awavumilie kwani wachimbaji hao wanaisaidia serikali kupunguza idadi ya vijana wasiokuwa na kazi mitaani.
" Kwa mfano, leseni yetu hii inawanufaisha zaidi ya watanzania 500 kwa kuwawezesha kujiajiri, na wengi kati ya watu hao ni vijana na Wanawake", alifafanua mkurugenzi huyo.
Aidha, Kapesya ameiomba serikali kuwasaidia wachimbaji wadogo kupata mikopo ya fedha kutoka taasisi za fedha nchini ambayo itawawezesha kununua vifaa vya kisasa vya upimaji na uchimbaji madini ili waweze kufanya kazi zao kwa uhakika na ufanisi.


.jpeg)

.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...