Na Janeth Raphael MichuziTv
Wizara ya Maliasili na Utalii, kupitia Mfuko wa Uhifadhi wa Wanyamapori Tanzania (TWPF), imeandaa Rasimu ya Mwongozo wa Uanzishaji na Usimamizi wa Maeneo ya Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori (Wildlife Management Areas – WMAs), ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuimarisha usimamizi wa maeneo hayo na kutatua changamoto zinazokabili jumuiya zinazoyasimamia.
Akifungua kikao kazi shirikishi cha kuandaa rasimu hiyo jijini Dodoma kwa niaba ya Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara hiyo, Bi. Kay Kagaruki, alisema hatua hiyo inatekeleza maelekezo ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, ya kuboresha mfumo wa usimamizi wa uhifadhi kwa kushirikiana na jamii kupitia WMAs.
Amesema Serikali imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa uhifadhi kuhakikisha maeneo hayo yanaendeshwa kwa ufanisi zaidi kupitia maboresho ya sera, miongozo na mifumo ya usimamizi inayolenga kuongeza manufaa kwa wananchi na kulinda rasilimali za wanyamapori.
"Serikali kupitia Wizara kwa kushirikiana na wadau wa uhifadhi imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha jumuiya za hifadhi kwa kutatua changamoto zinazozikabili na kuhakikisha zinafanya kazi kwa ufanisi zaidi," alisema Bi. Kagaruki.
Aidha, amewataka wananchi kuendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za uhifadhi, akisisitiza kuwa kulinda maliasili ni wajibu wa kila Mtanzania kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Kwa upande wake, Mratibu wa kikao hicho, Rose Mndendemi, alisema hadi sasa Tanzania ina jumla ya Maeneo ya Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori (WMAs) 24 yaliyopata idhini na haki ya matumizi ya rasilimali za wanyamapori, huku jumuiya nyingine 16 zikiwa katika hatua mbalimbali za kukamilisha taratibu za kupata haki hiyo.
Naye Afisa Wanyamapori wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Christopher Laizer, ameipongeza Wizara kwa kuwashirikisha wadau katika kuandaa rasimu ya mwongozo huo, akisema utakapokamilika utasaidia kuongeza ufanisi katika usimamizi wa WMAs na kuimarisha mchango wake katika maendeleo ya wananchi na uhifadhi endelevu wa rasilimali za taifa.
Kikao kazi hicho cha siku tatu kinawakutanisha maafisa kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Maafisa Wanyamapori wa Wilaya, viongozi wa Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya uhifadhi, kwa lengo la kukamilisha mwongozo utakaoboresha uanzishaji na usimamizi wa WMAs nchini.








.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...