Na Benny Mwaipaja, DURBAN

Nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zimeazimia kuharakisha mageuzi ya kiviwanda katika kanda, baada ya kuhitimisha Wiki ya Tisa ya Viwanda ya SADC (SIW 2026) iliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Durban, jimbo la KwaZulu-Natal, Afrika Kusini.

Zimesisitiza umuhimu wa kuimarisha minyororo ya thamani ya kikanda, kuharakisha uwekezaji wa kiviwanda, kutumia ubunifu na teknolojia mpya, pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Fedha na Ubia cha Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC), Bw. Zwelibanzi Sapula, alisema kuwa katika tathmini yake, mkutano ulibaini kuwa Ukanda wa Kusini mwa Afrika una rasilimali nyingi za asili, wajasiriamali wengi wanaokua na fursa kubwa za soko, lakini sekta ya viwanda haijatoa mchango mkubwa katika kuongeza mnyororo wa thamani katika rasilimali hizo.

Wajumbe walisisitiza kuwa ujenzi wa minyororo ya thamani ya kikanda iliyounganishwa kupitia ushirikiano katika kilimo, madini, dawa, uzalishaji wa magari, nguo na kemikali, ni muhimu kuongeza uongezaji thamani na kuimarisha ushindani wa viwanda vya SADC.

Vilevile, mabadiliko ya kidijitali, uchumi wa kijani, matumizi ya akili mnemba na teknolojia nyingine mpya vinabadilisha kwa kasi mifumo ya uzalishaji duniani, hivyo kuhitaji uwekezaji wa haraka kwenye miundombinu ya kidijitali na ya kijani, mifumo ya ubunifu, tafiti na uhawilishaji wa teknolojia.

Kilimo kilitajwa kuendelea kuwa nguzo muhimu ya mapinduzi ya viwanda, huku ukiwa na haja ya kuimarisha minyororo ya kiviwanda ya kilimo na kupanua sekta ya uchakataji wa mazao ili kuboresha usalama wa chakula, kuongeza mauzo nje na kutengeneza ajira, hasa kwa wanawake na vijana.

Utajiri wa madini muhimu wa kanda hiyo pia ulitajwa kuwa fursa ya kipekee ya kuiweka upya Kanda ya Kusini mwa Afrika kwenye minyororo ya kimataifa ya viwanda, kwa kuachana na uuzaji wa malighafi na badala yake kuwekeza kwenye uchakataji, uongezaji thamani na uzalishaji wa ndani.

Wajumbe pia walisisitiza kuwa wajasiriamali wadogo na wa kati ndio uti wa mgongo wa uchumi wa kikanda, hivyo upatikanaji wao wa mitaji, teknolojia, masoko, viwango na huduma za maendeleo ya biashara lazima uboreshwe.

Ilielezwa pia kuwa maendeleo endelevu ya viwanda hayawezi kufikiwa na serikali pekee, bali yanahitaji ushirikiano imara kati ya serikali, sekta binafsi, taasisi za fedha za maendeleo, wasomi na washirika wa maendeleo.

Wajumbe walihitimisha kuwa mafanikio ya ajenda ya uviwandishaji Kusini mwa Afrika yatategemea dhamira ya pamoja ya serikali, wafanyabiashara, taasisi za fedha, washirika wa maendeleo na wadau wote kubadilisha mapendekezo na ushirikiano uliojengwa wakati wa mkutano huo kuwa mipango halisi, uwekezaji na matokeo yanayopimika yatakayoboresha maisha ya wananchi wa kanda ya SADC.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...