Na Seif Mangwangi, Michuzi TV Arusha
WATUMISHI wa Wakala wa Vipimo nchini (WMA), wametakiwa kuhakikisha wanapambana ipasavyo na wafanyabiashara wahuni ambao wamekuwa wakiharibu vipimo kwa lengo la kuwaibia wanunuzi na kujipatia faida kubwa.
Aidha watumishi hao wametakiwa kuwa wazalendo kwa nchi hususani kwa bidhaa ambazo zimekwisha fungwa na kusafirishwa nje ya nchi kwa kuwa wakipitisha vipimo vilivyoharibiwa huiharibia nchi ndani na nje ya nchi.
Agizo hilo limetolewa leo Agosti 2, 2026, na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Dennis Lazaro Londo, katika ufunguzi wa baraza la 38 la wafanyakazi wa wakala wa vipimo nchini unaoendelea Jijini Arusha.
Londo amesema ni wakati wa wafanyakazi wa wakala wa vipimo kuwa wazalendo na kumuogopa Mungu ili kuwajengea imani Watanzania juu ya mashine za vipimo wanazozikagua na kuzipa ithibati.
" Itapendeza sana mtu akinunua bidhaa yake aridhike na kuwa na imani, ni wajibu wenu kuwa wazalendo na kuwajengea imani Watanzania, sio sawa mtu anaenda kununua bidhaa kwa ujazo fulani kumbe umeshapunguzwa kupitia kipimo kisichokuwa sahihi, nendeni mkapambane na wahuni wote wanaoharibu vipimo," amesema.
Amesema wanaosafirisha bidhaa nje ya nchi zikiwa pungufu wanaharibu taswira ya nchi na matokeo yake ni kupoteza uaminifu Kwa wateja na zaidi ni kuharibia vizazi vijavyo kwa kukosa masoko na hivyo kuikosesha nchi mapato.
Wakati huo huo Naibu Waziri Londo amewataka watumishi hao kutumia mpango mkakati wake mpya2027/2030 kuongeza uwajibikaji na kwamba watafakari nafasi ya mtumishi mmoja mmoja katika kudhibiti uhuni wa wafanyabiashara wachache.
Kamishna wa vipimo nchini, Alban Kihulla amesema kupitia mpango mkakati wake mpya wanaenda kuongeza imani kwa wananchi kupitia ukaguzi wa vipimo.
Aidha amesema wanaenda kushirikiana na sekta binafsi ili kuboresha utendaji wao wa kazi, kuboresha mazingira ya ofisi zao na kuboresha mpango wa mafunzo kwa watumishi.
Kihulla amesema kupitia mpango mkakati wa miaka mitano iliyopita wakala wa vipimo umeweza kuhakiki mizani milioni5.5 pamoja na kujenga ofisi 26 za wakala wa vipimo nchini.
Amesema changamoto kubwa wanayopambana nayo ni kuwepo kwa adhabu ndogo kwa wanaochakachua vipimo ambapo Kwa mujibu wa Sheria ya wakala wa vipimo sura namba 340 adhabu ni laki moja na isizidi milioni 20.



.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...