Na Mwandishi Wetu, Tanga
CHUO cha Elimu ya Biashara (CBE) kimesema kimeweka mfumo wa kuwawezesha wanafunzi kuendeleza mawazo na bunifu zinazolenga kutoa suluhisho kwa changamoto zinazowakabili wananchi.

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko wa CBE, Georgina Misama, amesema hayo kwenye Banda la chuo hicho katika Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu inayoendelea jijini Tanga.

Amesema kupitia wiki hiyo, CBE imekuwa ikitoa elimu kwa wananchi pamoja na kuonyesha bunifu mbalimbali zinazozalishwa na wanafunzi, huku chuo kikiwasimamia wanafunzi kuanzia hatua ya awali ya wazo hadi kukamilika kwa bunifu hizo.

“Chuo kimekuwa na mfumo wa kuendeleza bunifu na mawazo yanayotolewa na wanafunzi ambayo yana lengo la kutatua changamoto zinazowakabili wananchi,” amesema Georgina.

Kwa upande wake, mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa CBE, Amiri Sharifu, amebuni kifaa cha kidijitali kwa ajili ya wakaguzi wa mizani, kinachowawezesha kupata taarifa za mizani wanayoikagua moja kwa moja kupitia simu zao za mkononi.

Amesema mfumo huo unalenga kuondoa changamoto ya wakaguzi kutembea na vitabu vya karatasi nyingi wakati wa kujaza taarifa za ukaguzi wa mizani, huku pia ukipunguza muda unaotumika katika zoezi hilo.

“Kwa kutumia mfumo huu, mkaguzi anaweza kupata taarifa za mzani papo hapo kupitia simu yake ya mkononi bila kutegemea karatasi, jambo ambalo litasaidia kupunguza muda wa ukaguzi,” amesema Sharifu.

Naye mwanafunzi wa mwaka wa kwanza, Sambu Timothy, amebuni mfumo wa kidijitali unaojulikana kama Smart Mauzo, unaomsaidia mfanyabiashara kupata taarifa za mauzo ya biashara yake kupitia simu janja.

Amesema mfumo huo una uwezo wa kutambua wateja ambao hawajafanya manunuzi kwa muda mrefu na kuwawezesha wafanyabiashara kuwatumia ujumbe mfupi wa simu (SMS) ili kuwakumbusha kuhusu bidhaa au huduma zao.

Timothy amesema mfumo huo upo katika hatua za mwisho za kukamilishwa na baada ya hapo utaingizwa sokoni kwa lengo la kuwasaidia wafanyabiashara kutunza kumbukumbu za uwekezaji, mauzo na matumizi, hatua ambayo itawasaidia kukuza biashara zao.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...