Na Mwandishi Wetu, Tanga
MAMLAKA ya Elimu Tanzania (TEA) imesema mdau yeyote atakayechangia katika Mfuko wa Elimu wa Taifa, ataweza kupata fursa ya kuomba nafuu ya kodi kwa kutumia cheti cha utambuzi kinachotolewa na mamlaka hiyo.

Akizungumza katika Banda la TEA kwenye Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu inayoendelea katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara jijini Tanga, Afisa Mwandamizi wa TEA Joyce Minja amesema, wachangiaji wa Mfuko wa Elimu hupata manufaa mbalimbali kutokana na mchango wao katika kuendeleza sekta ya elimu.

Amesema miongoni mwa manufaa hayo ni kutambuliwa kwa mchango wao, kupata fursa ya kuomba nafuu ya kodi pamoja na kutangazwa ndani na nje ya nchi kama sehemu ya kuhamasisha wadau wengine kushiriki katika maendeleo ya elimu.

“Wachangiaji wa Mfuko wa Elimu wa Taifa, watapewa Cheti au Barua ya utambuzi wa uchangiaji elimu katika kusaidia maendeleo na uboreshaji miundombinu ya sekta ya elimu,” amesema Minja.

Ameongeza kuwa, cheti hicho kinaweza kutumika katika kuomba nafuu ya kodi kwa mujibu wa Kifungu cha 16(1) cha Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura ya 332, Toleo la 2019.

Aidha, amesema wachangiaji wataingizwa katika kanzidata ya wachangiaji wa Mfuko wa Elimu, hatua itakayosaidia kutunza kumbukumbu zao kwa kudumu na kuwezesha kutambua mchango walioutoa katika sekta ya elimu.

Kwa mujibu wa TEA, wachangiaji pia watapata fursa ya kutambuliwa na kutangazwa ndani na nje ya nchi, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha ushiriki wa wadau katika kusaidia maendeleo ya elimu.

Mfuko wa Elimu wa Taifa unalenga kuimarisha ushiriki wa wadau mbalimbali katika maendeleo ya sekta ya elimu kupitia michango na misaada inayolenga kuboresha mazingira na huduma za elimu nchini.

Amewataka wadau mbalimbali ,wakiwemo wafanyabiashara ,wenye viwanda ,Taasisi za Serikali, Sekta Binafsi mashirika ya ndani na nje ya nchi kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha miundombinu ya kujifinzia na kufundishia kwa kuchangia rasilimali fedha au vifaa kupitia Mfuko huo wa Elimu wa Taifa

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...