-HAPI AKUTANA NA RAIS DANIEL CHAPO WA MSUMBIJI, AWASILISHA SALAMU ZA MWENYEKITI WA CCM RAIS DKT. SAMIA SULUHU HASSAN

Chimoio, Msumbiji — Agosti 22, 2026.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Comrade Ally Salum Hapi, amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Msumbiji ambaye pia ni Rais wa Chama cha FRELIMO, Mhe. Daniel Francisco Chapo.

Mazungumzo hayo yamefanyika jijini Chimoio, Msumbiji, wakati Comrade Hapi akimwakilisha Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Asha-Rose Migiro, katika Kongamano la 11 la Kitaifa la Makada wa FRELIMO linaloongozwa na Rais Daniel Chapo.

Kongamano hilo ni sehemu ya maandalizi kuelekea Mkutano Mkuu wa Chama cha FRELIMO unaotarajiwa kufanyika mwaka 2027.

Katika mazungumzo hayo, Comrade Hapi amewasilisha salamu za kheri, udugu na ushirikiano kutoka kwa Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa Rais Chapo na chama cha FRELIMO.

Hapi amesema uhusiano kati ya CCM na FRELIMO ni wa kihistoria na wa kindugu, uliyojengwa tangu enzi za harakati za ukombozi wa Afrika, na umeendelea kuimarika katika nyanja mbalimbali.

Chama cha FRELIMO kilianzishwa jijini Dar es Salaam, Tanzania, tarehe 25 Juni 1962, wakati Tanzania ikiwa kitovu muhimu cha harakati za ukombozi wa mataifa ya Kusini mwa Afrika.

Uhusiano huo wa kihistoria umeendelea kuwa msingi muhimu wa ushirikiano kati ya Tanzania na Msumbiji, pamoja na vyama vya CCM na FRELIMO, katika kuendeleza mshikamano, amani na maendeleo ya wananchi wa nchi hizo mbili.

Mazungumzo ya Hapi na Rais Chapo yanaongeza msukumo katika kuendeleza uhusiano wa karibu kati ya vyama hivyo viwili vya ukombozi na kuimarisha ushirikiano wao kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...