NA MWANDISHI WETU
Historia kubwa imeandikwa Tanzania. Hii ni kufuatia kukamilika kwa mradi wa Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere (JNHPP), chenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115 katika eneo la mradi, wilayani Rufiji, mkoani Pwani.
Kukamilisha kwa mradi huo uliogharimu shilingi trilioni 7.452, kunachochea moja kwa moja maendeleo ya shughuli za kijamii na kiuchumi kupitia uzalishaji wa nishati ya umeme ambayo ni muhimu katika shughuli hizo.
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amezindua rasmi mradi huo Agosti 22, 2026 wilayani Rufiji.
Akitoa maoni yake kuhusiana na uzinduzi wa mradi huo, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Taifa, Mary Chatanda, amesema kama Rais Dk. Samia asingekuwa thabiti katika uongozi wake, mradi huo usingekamilika.
"Rais Dk. Samia alipoingia madarakani mwaka 2021, alikuta mradi huu umefikia utekelezaji wa asilimia 33, lakini ndani ya miaka mitano ya uongozi wake, mradi huo umekamilika wote na unazalisha megawati 2,115 za umeme," amesema Chatanda.
Amebainisha kuwa, uzalishaji wa megawati hizo unaleta uhakika kwa nchi yetu kujitosheleza kimahitaji na kuwa na uwezo wa kuuza ziada ya umeme nje ya nchi, na kuongeza pato la nchi.
"Mradi huu umechangia asilimia 44.9 za umeme katika Gridi ya Taifa, na hivyo unamaliza kabisa mahitaji ya umeme yaliyopo nchini, na hivyo kuwezesha shughuli za viwanda, biashara, uwekezaji, kilimo, utoaji wa huduma bora za kijamii kama elimu, afya, maji kufanikiwa kupitia upatikanaji wa umeme wa uhakika," amesema.
AMPONGEZA RAIS SAMIA KUTIMIZA NDOTO ZA HAYATI MWALIMU JULIUS NYERERE
Mwenyekiti huyo UWT Taifa amesema, kuzinduliwa mradi huo, kunatimiza ndoto za zaidi ya miaka 50 za Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliyetamani mradi huo ukamilike.
"Agosti 22, 2026, inabaki siku ya kihistoria nchini kwani ndoto za Hayati Mwalimu Nyerere zimetimia. Hayati Dk. John Magufuli alifufua ndoto hizo, lakini mama yetu Dk. Samia amekamilisha, na sasa si ndoto tena bali ni kitu halisi," ameongeza.
Ikumbukwe kuwa, mradi huo una mitamboni tisa ya uzalishaji ambayo yote inafanya kazi. Aidha, Tanzania imeweka historia ya aina yake barani Afrika na ulimwenguni kwa kuwa na uhakika wa nishati ya umeme kwa mahitaji ya ndani na kuwa na ziara ya kuuza nje ya nchi.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...