Kamishana wa kamisheni ya Polisi Jamii nchini, CP Alex Mkama amewataka maafisa, wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali wa Jeshi la Polisi kuendelea kuzingatia maadili na kudumisha nidhamu wanapotekelezaji wa majukumu yao ili kujenga uhusiano mzuri na jamii. Pia amewataka kutofanya kazi kwa mazoea kutokana na mabadiliko ya kasi ya uhalifu.
CP Mkama ametoa maagizo hayo leo Jumamosi Agosti 22, 2026, wakati wa maadhimisho ya miaka 15 ya utumishi wa umoja wa askari wa Jeshi la Polisi waliohitimu depo mwaka 2011/2012 (GH Tanzania) huku akidokeza kuwa wananchi wamekuwa wakilalamikia maadili ya baadhi ya maafisa wakaguzi na askari.
“Askari lazima awe na maadili wakati wote. Wananchi wamekuwa wakilalamikia maadili ya baadhi ya maafisa wakaguzi na askari, hivyo ili tuwe na mahusiano mazuri na wananchi lazima maadili yawe mazuri. Tuyaenzi maadili ya afisa wa polisi,” amesema Cp Mkama
Amesema nidhamu ni msingi wa jeshi lolote duniani, akiwataka askari kuhakikisha wanazingatia misingi hiyo wakati wote huku akidokeza kuwa mabadiliko ya dunia yamechangia kubadilika kwa mbinu za uhalifu.
Awali, akiwasilisha hotuba ya GH Tanzania, mlezi wa kundi hilo, ASP Mabuba Malima amesema umoja huo umeendelea kujikita katika kusaidiana wakati wa changamoto na kurudisha kwa jamii.
Amesema wanachama hao wa GH Tanzania wametoa msaada wa zaidi ya Sh11 milioni kwa watoto wanaosoma katika Shule ya Wanafunzi Wenye Mahitaji Maalum ya Mitindo wilayani Misungwi, yakiwemo madawati 53, magodoro 100, mashuka 200, mchele kilo 200, mafuta ya kupikia lita 60, debe moja la maharage pamoja na mahitaji mengine muhimu.
Malima amesema GH Tanzania ilianzishwa na wanachama wa depo ya mwaka 2011/2012 baada ya kutawanywa katika vituo mbalimbali vya kazi Machi 30, 2012, ikianza na wanachama 75 na sasa ikiwa na zaidi ya wanachama 1,500 Tanzania Bara na Visiwani.
“Wanachama walianza kwa kuchangishana Shilingi 5,000 pekee, lakini kwa sasa umoja huo umekuwa ukitoa zaidi ya Sh7 milioni kwa mwanachama anayepatwa na msiba wa mzazi, mtoto au mwenza,” amesema Malima.
Aidha, amesema zaidi ya Sh15 milioni hutolewa kwa ndugu wa mwanachama aliyefariki au mwanachama anayefukuzwa kazi ili kumsaidia kujikimu huku kila ifikapo Agosti 15, wanachama hao hutenga muda wa kufanya shughuli za kijamii badala ya kusherehekea peke yao, zikiwemo kutembelea wagonjwa hospitalini, kufanya usafi katika masoko na stendi, kutembelea vituo vya watu wenye mahitaji maalum pamoja na kushiriki michezo na burudani.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Polisi Wanamaji Mwanza, SACP Ndagile Makubi amesema maboresho yanayoendelea ndani ya Jeshi la Polisi yanaonekana kupitia ushirikiano wa askari katika shughuli mbalimbali za kijamii.







Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...