Na Mwandishi Wetu

BENKI ya DCB Commercial Bank Plc imemtangaza Dkt. Charles Stephen Kimei kuwa Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Wakurugenzi, akitarajiwa kutumia uzoefu wake wa zaidi ya miaka 40 katika sekta ya benki, sera za fedha, udhibiti, utafiti wa uchumi na utawala bora.

Dkt. Kimei ni miongoni mwa viongozi wenye uzoefu mkubwa katika sekta ya benki na fedha nchini Tanzania, ambapo alianza safari yake ya kitaaluma katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), akishika nyadhifa mbalimbali za juu ikiwamo Mkurugenzi wa Usimamizi wa Benki pamoja na Mkurugenzi wa Utafiti na Sera za Kiuchumi.

Baadaye aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji na Afisa Mtendaji Mkuu wa CRDB Bank Plc, nafasi aliyoitumikia katika kipindi ambacho taasisi hiyo ilifanya mabadiliko makubwa kutoka benki ya ushirika na kuwa benki ya biashara yenye ushindani mkubwa.

DCB Commercial Bank imesema uzoefu wa Dkt. Kimei katika mabadiliko ya taasisi, masoko ya fedha, usimamizi na utawala bora utakuwa muhimu katika hatua ambayo benki hiyo inaendelea kuimarisha shughuli zake na kuongeza thamani kwa wateja, wanahisa na wadau wengine.

Mbali na nafasi zake za kiutendaji, Dkt. Kimei amewahi kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi na uwakilishi katika taasisi za ndani na nje ya sekta ya benki, zikiwamo Tanzania Bankers Association, Swissport Tanzania Plc, Economic and Social Research Foundation (ESRF), Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Tanzania Education Authority.

Kutokana na mchango wake katika sekta ya benki na fedha, Dkt. Kimei amewahi kutunukiwa tuzo mbalimbali, ikiwamo East Africa Banker Lifetime Achievement Award mwaka 2016.

DCB Commercial Bank imesema uteuzi huo unafungua ukurasa mpya wa uongozi wa benki hiyo, ukiwa na msukumo wa kuimarisha mabadiliko, ubunifu, ukuaji endelevu na uundaji wa thamani kwa benki, wateja, wanahisa na wadau wake.

Uteuzi wa Dkt. Kimei unatarajiwa kuongeza nguvu katika uongozi wa kimkakati wa DCB, kutokana na uzoefu wake mpana katika sekta ya fedha, udhibiti wa benki na usimamizi wa taasisi.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...