Na Mwandishi Wetu
BAADHI ya Wananchi wa Dar es Salaam hususani watumiaji wa usafiri wa Mabasi wametetea utaratibu wa Mabasi hayo kutoa huduma maeneo mengine tofauti na Kituo cha Mabasi cha Magufuli na kuutaka Uongozi wa Mkoa kulitafakari upya suala hilo.
Awali mapema wiki hii Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila alitoa muda wa wiki moja hadi Agosti 21 Mwaka huu kwa mabasi yote yanayotoa huduma tofauti na Kituo cha Mabasi cha Magufuli kuondoka katika maeneo hayo na kurejea kituoni hapo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti tangu kutolewa kwa agizo hilo, wananchi hao hususani watumiaji wa huduma hizo za Usafiri wamesema agizo hilo la Mkuu wa Mkoa lina lengo la kuwarejesha kwenye kadhia waliyokuwa wakiipata awali.
Wamesema kulingana na jiografia ya Jiji la Dar es Salaam ni changamoto kubwa kwa abiria kutoka maeneo mbalimbali kupata 'urahisi' wa kwenda Mbezi kwa ajili ya kusafiri hususani nyakati za usiku ambapo mara nyingi usafiri huwa shida na wakati mwingine tatizo la foleni.
" Hakuna ubishi kuwa uwepo wa huduma hizi maeneo tofauti na Mbezi (Magufuli) umetusaidia kuondoa changamoto nyingi, mbali na usumbufu unaotokana na kero za wapiga debe, suala la umbali wa kukifikia kituo hicho ilikuwa ni tatizo jingine" amesema mmoja wa wananchi aliyejitambulisha kwa jina la Seif Juma
Amesema ni vyema uongozi wa Mkoa ukalitafakari upya suala hilo hasa Kipindi hiki ambapo pia safari nyingi za Mabasi zinafanyika usiku kwa madai kwamba uwepo wa 'vituo vidogo' hivyo mitaani vinasaidia kuepusha usumbufu kwa abiria ikiwemo kuepuka kuibiwa mizigo na mali zao.
Naye mwananchi Emmanuel Yesaya, abiria aliyekuwa safarini kuelekeza Mkoa wa Katavi, amesema imekuwa nafuu sana kwa wageni kutoka Mkoani kwa uwepo wa 'vituo vidogo' hivyo mitaani kwani imekuwa ikiwaondolea usumbufu Mkubwa kutokana na ugeni wao.
Amesema kwa mgeni ambaye mara ya kwanza anashuka Mbezi hukumbana na 'adha' kubwa ikiwemo usafiri kwenda eneo alilokusudia akisisitiza kuwa uwepo wa Mabasi hayo yanayopakia na kushusha mbali na Kituo cha Magufuli umeiondoa kabisa changamoto hiyo.
Wamesema tangia kuanza kwa huduma hizo, kwa kiasi kikubwa kumesaidia abiria wengi kuondokana kero zikiwemo za kupoteza mizigo yao sambamba na kero ya usafiri kutoka maeneo watokayo kwenda Kituo Cha Magufuli huku pia wakiitumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali kwa kuruhusu uwepo wa 'vituo hivyo miaka michache iliyopita.
Hata hivyo Uongozi wa Chama Cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania(TABOA) haukupatikana kulizungumzia suala hilo huku ikielezwa kuwa Utaratibu wa uwepo wa vituo hivyo mitaani ulitokana na Baraka za Serikali huku Mamlaka ya Usimamizi wa Huduma za Usafiri nchini (LATRA) ikiweka utaratibu wa utoaji wa vibali vya Mabasi kutoa huduma hizo katika maeneo hayo.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...