Na Mwandishi Wetu, Dodoma
CHUO cha Bahari Dar es Salaam (DMI) kimesema Tanzania inahitaji kuongeza idadi ya wataalamu wa usafirishaji, lojistiki na usimamizi wa mnyororo wa usambazaji wa bidhaa ili kuongeza tija, ushindani wa bidhaa za ndani na kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Mkuu wa DMI, Profesa Tumaini Gurumo, amesema pamoja na chuo hicho kujulikana kwa kutoa mafunzo yanayohusiana na masuala ya bahari na mabaharia, pia kinatoa mafunzo ya lojistiki na usimamizi wa mnyororo wa usambazaji wa bidhaa, ambayo ni muhimu katika kukuza biashara na uchumi.
Profesa Gurumo aliyasema hayo wakati alipotembelea Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo na Ufugaji Nane Nane yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Samwel Malecela, Nzuguni, Dodoma.
Amesema kilimo na shughuli za bahari haviwezi kutenganishwa kwa kuwa mazao yanayozalishwa nchini yanahitaji mifumo bora ya usafirishaji ili kuwafikia walaji na masoko kwa wakati na kwa gharama zinazokubalika.
“Tunapozungumzia biashara shindani, tunahitaji wataalamu katika maeneo mbalimbali, likiwemo hili la lojistiki za usafirishaji wa mazao, mifugo, abiria na bidhaa nyingine,” amesema.
Amesema Tanzania ikiongeza uzalishaji wa mazao bila kuwa na wataalamu na mifumo bora ya kuyasafirisha, juhudi hizo zinaweza kukosa tija kutokana na changamoto za kuyafikisha katika masoko kwa wakati.
Kwa mujibu wa Profesa Gurumo, uwepo wa wataalamu wenye ujuzi katika mnyororo wa usafirishaji ni sehemu muhimu ya maandalizi ya Tanzania kushindana katika masoko ya kimataifa, kwa kuwa ushindani wa kiuchumi hauishii ndani ya mipaka ya nchi.
“Tunapozungumzia biashara shindani au uchumi shindani, maana yake si kushindana ndani ya nchi pekee, bali tunautazama ushindani wa kimataifa,” amesema.
Amesema DMI imeendelea kuboresha mitaala yake ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia, ikiwemo matumizi ya mifumo ya kidijitali na akili bandia (AI) katika sekta ya usafirishaji.
Amesema maboresho hayo yanalenga kuhakikisha wahitimu wanaingia katika soko la ajira wakiwa na ujuzi unaoendana na mahitaji ya sasa ya sekta ya usafirishaji na uchumi kwa ujumla.
“Tunapotengeneza mitaala yetu tumeibadilisha na sasa kila mtaalamu mpya anahusisha masuala ya kidijitali pamoja na AI,” amesema.
Mbali na maboresho ya mitaala, amesema DMI imeongeza na kuboresha vifaa vya kufundishia ili kuwawezesha wanafunzi kupata ujuzi unaoendana na teknolojia zinazotumika katika sekta ya usafirishaji.
Profesa Gurumo amesema chuo hicho pia kinaendelea kushirikiana kwa karibu na wadau wa sekta ya usafirishaji na viwanda ambako wahitimu wake huenda kufanya kazi, jambo linalokisaidia chuo kufahamu mabadiliko ya mahitaji ya soko la ajira.
Amesema ushirikiano huo pia unawapa walimu fursa ya kujifunza teknolojia mpya na kuzitumia katika kuboresha mitaala pamoja na vifaa vya kufundishia.
Katika maonesho hayo, Profesa Gurumo amesema DMI imeendelea kutoa elimu kwa wananchi na vijana kuhusu fursa za mafunzo yanayotolewa na chuo hicho, huku akiwataka vijana kuzitazama sekta za bahari, usafirishaji na lojistiki kama maeneo yenye fursa za ajira na kujiajiri.
“Tunatambua kwamba vijana wamechukua sehemu kubwa ya idadi ya watu nchini. Lazima wapate elimu na ujuzi na wajue kwamba kuna sekta ambazo wana uwezo wa kuzifanyia kazi na kupata weledi utakaowasaidia kupata ajira na kupeleka maendeleo ya nchi yetu mbele,” amesema.



.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...