Na Farida Saidi Morogoro
Wanafunzi 6,800 kutoka nchi tano za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wamewasili mkoani Morogoro kushiriki Mashindano ya Michezo ya Wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (FEASSA) 2026, yanayotarajiwa kuanza rasmi kesho, Agosti 12, hadi Agosti 23, mwaka huu.
Mashindano hayo, yanayofanyika kwa mara ya 23 katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na mara ya tano nchini Tanzania, yatawakutanisha wanafunzi kutoka Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Morogoro, Mkuu wa Mkoa huo, Adam Kighoma Malima, amesema Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), imejipanga kuhakikisha mkoa huo unakuwa mwenyeji bora wa mashindano hayo.
Amesema jumla ya viwanja 21 pamoja na maeneo manane ya malazi vimetengwa kwa ajili ya washiriki wa mashindano hayo.
Malima amewahakikishia washiriki kuwa ulinzi na usalama umeimarishwa vya kutosha, huku akiwataka wananchi wa Morogoro kuchangamkia fursa za kiuchumi zitakazotokana na ujio wa maelfu ya wageni.
Aidha, amewataka wakazi wa mkoa huo kuwakaribisha wageni kwa ukarimu na kutumia mashindano hayo kujenga mahusiano mazuri kati ya Tanzania na nchi nyingine wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Amesema Tanzania itawakilishwa na wanafunzi 1,510 kutoka mikoa 26 ya Tanzania Bara, ikiwa ni idadi kubwa zaidi ya washiriki kutoka nchini humo katika historia ya mashindano hayo.
Kwa upande wa Morogoro, Malima amesema mkoa huo utashiriki katika michezo 13 baada ya kufanya vizuri katika mashindano ya UMISSETA na UMITASHUMTA yaliyofanyika mkoani Iringa Juni mwaka huu.
Kwa ujumla, FEASSA 2026 itahusisha michezo 20 kwa wanafunzi wa shule za sekondari, michezo sita kwa shule za msingi na michezo minne kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Malima amesema ujio wa maelfu ya washiriki na wageni unatoa fursa kubwa kwa wananchi kunufaika kiuchumi kupitia biashara, usafiri, chakula, malazi na huduma mbalimbali.
Ameongeza kuwa mashindano hayo pia yatatoa fursa ya kutangaza vivutio vya utalii vya Morogoro na Tanzania kwa ujumla kwa wageni kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki.
Ufunguzi rasmi wa mashindano hayo unatarajiwa kufanyika Agosti 16, ambapo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kushuhudia mashindano hayo na kuwakaribisha wageni kwa ukarimu, huku akivitaka vyombo vya habari kutumia fursa hiyo kuitangaza Morogoro na Tanzania kwa ujumla.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...