Na Mwandishi Wetu, Tanga
CHUO cha Kodi (ITA) kimeshiriki Maonesho ya Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yanayoendelea katika Viwanja vya Usagara jijini Tanga, kwa kutoa elimu kuhusu majukumu ya Chuo hicho pamoja na fursa za mafunzo zinazotolewa.
Wanafunzi na wadau mbalimbali waliotembelea banda la ITA wamepata fursa ya kufahamu kwa kina kuhusu programu za mafunzo zinazotolewa na Chuo hicho, huku wakihamasishwa kujiunga na mafunzo hayo.
Maonesho hayo yaliyoanza Agosti 15, 2026, yamekuwa pia jukwaa kwa ITA kuwaelimisha wananchi kuhusu nafasi ya taaluma mbalimbali katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na maeneo mengine ya ajira.
Akizungumza na wanafunzi waliotembelea banda hilo, Afisa Mkuu wa Uhusiano wa Umma wa ITA, Oliver Njunwa, amesema mwanafunzi anayelenga kufanya kazi TRA anapaswa kuzingatia masomo yote kwa kuwa Mamlaka hiyo inaajiri wataalamu wenye taaluma mbalimbali.
“TRA ina wafanyakazi wenye taaluma mbalimbali, hivyo mwanafunzi anatakiwa kuzingatia masomo yote na kufanya vizuri katika masomo yake,” amesema Njunwa.
Aidha, amewataka wanafunzi wanaotaka kusoma ITA kutokuwa na mtazamo wa kwamba mhitimu wa Chuo hicho anapaswa kufanya kazi TRA pekee, bali kuwa tayari kufanya kazi katika taasisi au maeneo mengine ambako taaluma zao zinahitajika.
“Mwanafunzi aliyesoma ITA anajengwa kufanya kazi sehemu yoyote ambayo taaluma aliyoisomea inahitajika pamoja na kujiajiri,” amesema.
Maonesho ya Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yanaendelea katika Viwanja vya Usagara jijini Tanga hadi Agosti 24, 2026.


.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...