Na Mwandishi Wetu, Dodoma
MSULUHISHI wa Migogoro ya Bima (TIO) amewataka wakulima waliokata bima za kilimo kupitia benki au mawakala wa bima, kutumia Ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima pale wanapokumbana na migogoro ya fidia ili kupata haki zao badala ya kukimbilia mahakamani.

Akizungumza katika Maonesho ya Kilimo ya Kimataifa Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Samwel Malecela jijini Dodoma, Msuluhishi Mkuu wa TIO Aloyce Mbunito, alisema ofisi hiyo iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria Sura ya 394 ina jukumu la kutatua migogoro ya bima kwa njia mbadala ya mahakama.

Alisema ofisi hiyo pia inalenga kulinda watumiaji wa huduma za bima na kuongeza imani ya wananchi katika sekta hiyo.

Mbunito alisema migogoro inayopokelewa mara nyingi inahusisha kukataliwa kwa madai ya fidia, kulipwa fidia isiyolingana na hasara halisi, kucheleweshwa kwa majibu ya madai pamoja na kutokuelewana kuhusu tafsiri ya mikataba ya bima.

Alisema tangu ofisi hiyo ianze kazi mwaka 2025, imefanikiwa kutatua zaidi ya migogoro 2,015, jambo alilosema linaonyesha kuwa wananchi wameanza kutambua umuhimu wa kuitumia kupata haki zao wanapokumbana na changamoto katika huduma za bima.

Aidha, Mbunito alisema katika maonesho hayo wamepokea viongozi wa vyama vya ushirika vya wakulima kutoka mkoani Mara, waliowasilisha changamoto zinazowakabili wakulima wa tumbaku waliopata hasara kutokana na mvua ya mawe, licha ya kuwa walikuwa wamekata bima kupitia benki.

Kwa mujibu wa Mbunito, changamoto kubwa iliyobainika ni baadhi ya wakulima kutofahamu kampuni za bima zilizowahudumia kwa kuwa walikata bima kupitia benki zilizokuwa mawakala wa kampuni hizo.

Alisema pia baadhi ya wakulima hawana mikataba ya bima, ambayo ni nyaraka muhimu katika kufuatilia madai ya fidia pale wanapopata hasara.

Naye Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Mara (WAMACU), Momanyi Range, alisema elimu waliyoipata katika banda la Ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima imewafungua macho kuhusu umuhimu wa kuwa na mikataba ya bima pamoja na kuhifadhi ushahidi wa majanga.

Alisema ushahidi huo unaweza kujumuisha picha za mazao yaliyoharibiwa na majanga, hatua ambayo inaweza kusaidia kurahisisha mchakato wa madai ya fidia.

Range alisema chama hicho sasa kitawaongoza wakulima walioathiriwa kukusanya malalamiko yao, kupata mikataba ya bima kutoka benki husika na kuyawasilisha katika Ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima ili kuhakikisha wanapata haki zao.

Alisema hatua hiyo itasaidia kuwawezesha wakulima kukabiliana na hasara zinazotokana na majanga na kuendelea na shughuli za uzalishaji bila kuathiriwa zaidi na athari za majanga hayo.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...