MRADI wa Mafunzo ya Kitaaluma ya Ufundi Stadi katika Sekta ya Migodi (IMTT) umeendelea kuwa daraja muhimu kwa vijana kupata ujuzi unaohitajika katika sekta ya migodi, huku mfumo wake wa Uanagenzi ukiwawezesha wanafunzi kujifunza darasani na kufanya kazi za vitendo katika migodi, hatua inayochangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ya kujenga uchumi jumuishi unaoshirikisha wananchi katika shughuli za uzalishaji.

Akizungumza na Michuzi TV katika Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu inayoendelea jijini Tanga kuanzia Agosti 15 hadi 24, Mkufunzi na Mratibu wa Uanagenzi wa IMTT kutoka VETA Moshi, mkoani Kilimanjaro, Mwl. John Nathan, amesema mpango huo ulianzishwa kwa ushirikiano kati ya VETA na Chemba ya Migodi Tanzania yaani (TCM).

Amebainisha kuwa tofauti na mafunzo ya kawaida ya darasani, mradi wa IMTT unafanyika katika mazingira mawili muhimu ni chuoni na katika eneo la kazi kwa maana ya viwandani, na Mfumo huo unamwezesha mwanafunzi kupata maarifa ya kinadharia na ujuzi wa vitendo kwa wakati mmoja, hivyo anapohitimu huwa tayari ana uzoefu wa mazingira halisi ya kazi.

“Anapokwenda kwenye kazi, anakuwa si mgeni tena, hahitaji uzoefu mwingine wa ziada ili kukidhi mahitaji ya ajira kwa sababu tayari ana uzoefu uliojengwa kutokana na muundo wa mafunzo".

Amesema kwa sasa, IMTT inatolewa katika chuo cha VETA Moshi peke yake, hii ni baada ya tafiti za awali zilifanyika na kubaini kuwa chuo hicho kilikuwa na mazingira, vifaa na miundombinu iliyohitajika kuendesha mafunzo hayo. Hata hivyo baadhi ya kampuni za migodi zimekuwa zikisaidia vijana kutoka maeneo yanayozunguka migodi kusafiri hadi Moshi kwa ajili ya mafunzo kabla ya kurejea katika maeneo yao ya kazi.

Ameeleza kuwa kwa mtu yeyote anayehitaji kujiunga na IMTT anatakiwa kuwa na ufaulu wa Kidato cha Nne na kuwa mzawa wa Tanzania na taarifa zaidi kuhusu taratibu za kujiunga wanaweza kufika VETA Moshi au kupata taarifa kupitia tovuti ya VETA.

Kwa upande wa mafanikio, amesema zaidi ya vijana 1,668 wamepatiwa mafunzo kupitia IMTT tangu kuanzishwa kwake mwaka 2009, ambapo asilimia 79.1 wameajiriwa katika migodi mbalimbali nchini, huku asilimia 1.1 wamepata ajira katika migodi nje ya nchi hali inayoonesha kuwa mafunzo ya ufundi stadi yanaweza kuwa njia muhimu ya kuwawezesha vijana kupata ajira.

Akieleza mchango wa programu hiyo katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, amesema IMTT inawawezesha vijana kushiriki moja kwa moja katika sekta ya migodi kwa kuwapatia ujuzi unaowawezesha kuwa sehemu ya nguvu kazi yenye tija, ambapo ajira wanazopata vijana hao haziwanufaishi wao pekee, bali pia familia zao na jamii zinazowazunguka.

Aidha, amegusia mabadiliko ya teknolojia katika sekta ya migodi yameifanya VETA kuendelea kuboresha mitaala ili kukidhi mahitaji mapya, hususan katika uchimbaji wa chini ya ardhi, amesema wanatarajia kuja na Programu sita mpya ambazo ni Scoop Operation, Tele-remote Bogger Operation, Cubex Operation, Jumbo Operation, Lifting and Rigging pamoja na Mobile Charging Unit Operation ili kuongeza ujuzi wa vijana wataokwenda kuisaidia sekta ya migodi kikamilifu kulingana na kasi ya ukuaji wa teknolojia.

Akitoa ujumbe kwa vijana wanaotembelea Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu inayofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara jijini Tanga, aliwataka kutumia fursa hiyo kupata taarifa kuhusu mafunzo ya ufundi stadi na kuchukua hatua badala ya kubaki na ndoto bila kuzifanyia kazi.

“Usiwe na wazo kichwani ukabaki na wazo, fanyia kazi, anza sasa,” akieleza kuwa vijana waliopitia IMTT wameweza kufikia fursa mbalimbali za ajira ndani na nje ya nchi, jambo linaloonesha kuwa ujuzi wa ufundi unaweza kuwa msingi wa mafanikio ya kiuchumi kwa vijana.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...