Na Mwandishi Wetu
JUMUIYA ya Wanawake katika Nyuklia Tanzania (WiNTz) imetembelea Hospitali ya KCMC na kufanya mazungumzo na wanawake wanaofanya kazi katika Kitengo cha Tiba ya Mionzi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Jumuiya hiyo kuwawezesha wanawake katika sekta ya sayansi na teknolojia ya nyuklia kupata fursa za masomo na mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu ndani na nje ya nchi.

Ziara hiyo imelenga pia kuwajengea uwezo wanawake wanaofanya kazi katika eneo la tiba ya mionzi kwa kuwafungulia fursa mbalimbali za kitaaluma zitakazowawezesha kuongeza maarifa na ujuzi katika taaluma zao na hivyo kuboresha zaidi huduma wanazozitoa kwa wananchi.

WiNTz, inayoongozwa na Rais wake ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC), Prof. Najat Kassim Mohammed, imeendelea kutekeleza programu mbalimbali zinazolenga kuongeza ushiriki wa wanawake na wasichana katika sayansi na teknolojia ya nyuklia nchini.

Miongoni mwa maeneo ambayo Jumuiya hiyo imekuwa ikiyapa kipaumbele ni kuhamasisha wasichana kusoma masomo ya sayansi, kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa uchunguzi wa saratani mapema, pamoja na kuwaunganisha wanawake wanaosoma na kufanya kazi katika taaluma za sayansi na fursa za masomo, tafiti na mafunzo ya kitaaluma ndani na nje ya Tanzania.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkaguzi wa Vyanzo vya Mionzi kutoka Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC), Bi. Lucy Lway, amesema pamoja na kukutana na wanawake wanaofanya kazi katika Kitengo cha Tiba ya Mionzi, WiNTz imetumia ziara hiyo kuwafariji watoto wanaopata matibabu ya saratani katika Hospitali ya KCMC.

Amesema Jumuiya hiyo inaamini kuwa pamoja na kuendeleza taaluma na kuwajengea uwezo wanawake katika sekta ya nyuklia, ni muhimu pia kutumia nafasi hiyo kuigusa jamii, hususan wagonjwa wanaopitia vipindi virefu vya matibabu.

Kwa upande wake, Mtaalamu wa Maabara kutoka TAEC, Bi. Hellen Kiyengo, amesema kujenga uelewa sahihi kuhusu teknolojia ya nyuklia ni muhimu katika kuisaidia jamii kufahamu matumizi na manufaa yake katika maisha ya kila siku, ikiwemo nafasi yake katika sekta ya afya.

Amesema elimu sahihi inasaidia pia kuondoa dhana potofu kuhusu teknolojia ya nyuklia na kuwajengea wananchi uelewa wa umuhimu wa kuzingatia usalama wakati wa matumizi ya mionzi.

Naye Msimamizi wa Wodi ya Watoto wanaopata matibabu ya saratani katika Hospitali ya KCMC, Bwn. Robert Kessy, ameipongeza WiNTz kwa kutenga muda wa kuwatembelea watoto wanaopata matibabu ya saratani, akisema baadhi yao hulazimika kukaa hospitalini kwa muda mrefu kutokana na aina na hatua mbalimbali za matibabu wanayopatiwa.

Amesema kutembelewa na kupata faraja kutoka kwa watu na taasisi mbalimbali kunasaidia kuwapa moyo watoto hao pamoja na wazazi na walezi wao katika kipindi cha matibabu.

“Watoto hawa wanakaa hospitalini kwa muda mrefu wakipatiwa matibabu. Kitendo cha Jumuiya ya Wanawake katika Nyuklia Tanzania kutenga muda na kuja kuwaona ni jambo jema kwa sababu kinawapa moyo watoto pamoja na wazazi wao,” amesema Kessy.

Kwa upande wake, Daktari kutoka Kitengo cha Tiba ya Mionzi KCMC, Dkt. Vaileth Mteta, ameishukuru WiNTz kwa kukutana na wanawake wanaofanya kazi katika kitengo hicho, akisema hatua hiyo imewapa nafasi ya kufahamu zaidi kuhusu Jumuiya hiyo pamoja na fursa zinazoweza kupatikana kupitia mtandao wa wanawake wanaofanya kazi katika maeneo ya sayansi na teknolojia ya nyuklia.

Amesema mkutano huo umeongeza pia hamasa ya kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa uchunguzi wa saratani mapema na kuwahi kupata matibabu kabla ugonjwa haujaenea na kufikia hatua ambazo matibabu yake yanaweza kuwa magumu zaidi.

Aidha, amesema wanawake wanaofanya kazi katika Kitengo cha Tiba ya Mionzi wamepata fursa ya kufahamu namna wanavyoweza kujiunga na WiNTz na kutumia mtandao huo kujenga mahusiano ya kitaaluma, kubadilishana uzoefu na kufikia fursa mbalimbali za mafunzo na maendeleo ya taaluma.

Ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za WiNTz za kujenga mtandao mpana wa wanawake katika sayansi na teknolojia ya nyuklia nchini, huku ikisisitiza umuhimu wa kuwajengea uwezo wanawake waliopo katika sekta hiyo na kuandaa kizazi kipya cha wasichana wenye ari ya kusomea masomo ya sayansi.

Kupitia shughuli hizo, WiNTz inalenga kuhakikisha wanawake wanasayansi nchini hawapati tu nafasi ya kushiriki katika maendeleo ya teknolojia ya nyuklia, bali pia wanakuwa sehemu muhimu ya kutumia sayansi hiyo katika kutatua changamoto za jamii, hususan katika afya, utafiti na maendeleo ya Taifa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...