Na Karama Kenyunko, Michuzi Tv
CHUO Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kimeanzisha kitengo maalumu cha matibabu ya meno kwa watoto wanaohitaji dawa za usingizi au ganzi, ikiwa ni sehemu ya ushirikiano kati ya MUHAS, Chuo Kikuu cha Ankara na Shirika la Ushirikiano na Uratibu la Türkiye (TİKA).

Makamu Mkuu wa MUHAS, Prof. Apollinary Kamuhabwa, amesema hayo leo Agosti 18, 2026, Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa kitengo hicho sambamba na kusainiwa kwa hati ya makubaliano (MoU) kati ya taasisi hizo.

Amesema kitengo hicho kilichoanzishwa katika Shule ya Meno ya MUHAS kimeanza kutoa huduma kwa watoto wenye matatizo ya kinywa na meno ambao hawawezi kufanyiwa matibabu wakiwa macho, huku watoto 27 wakiwa tayari wamepatiwa huduma tangu Mei mwaka huu.

Prof. Kamuhabwa amesema huduma hiyo ni muhimu kwa watoto wanaoogopa sindano, wasioweza kuvumilia matibabu ya meno wakiwa macho au wenye changamoto za kiafya zinazofanya matibabu ya kawaida kuwa magumu.

Amesema huduma hiyo haikuwahi kupatikana nchini, hivyo ushirikiano huo umeleta hatua muhimu katika kuongeza huduma za kibingwa kwa watoto.

“Wataalamu wa MUHAS, wakiwemo madaktari wa meno, wataalamu wa usingizi na ganzi, maabara na wauguzi, wamekwenda Chuo Kikuu cha Ankara kwa mafunzo, huku wataalamu kutoka Türkiye wakifika Tanzania kwa ajili ya kujenga uwezo wa wataalamu wa ndani,” amesema.

Pia TİKA na Chuo Kikuu cha Ankara vimeunga mkono mpango huo kwa kutoa vifaa tiba na utaalamu, huku hatua inayofuata ikiwa ni kuongeza wataalamu, vifaa na kupanua huduma ili watoto wengi zaidi wanufaike.

Mkurugenzi wa TİKA nchini Tanzania, Halim Ömer, amesema TİKA imewezesha kitengo hicho kwa kutoa vifaa vya ganzi, meno, kusaidia njia ya hewa kwa watoto, vifaa vya kupumulia na vifaa vya huduma za dharura

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ankara, Prof. Dkt. Necdet Ünüvar, amesema kuanzishwa kwa kitengo hicho ni hatua muhimu katika kuimarisha uhusiano wa kitaaluma na kitaalamu kati ya taasisi hizo, huku akiahidi kupanua ushirikiano katika sayansi za afya.

Mkuu wa Shule ya Meno ya MUHAS, Prof. Ferdinand Machibya, amesema ushirikiano huo unaweza kupanuliwa katika utafiti wa pamoja, mafunzo ya uzamili, kubadilishana wanafunzi na wataalamu, matumizi ya akili bandia katika uchanganuzi wa picha za kitabibu, kujenga uwezo wa huduma za tiba na kuandaa maombi ya pamoja ya ruzuku.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...