Na Janeth Raphael - MichuziTv .
WAKATI Tanzania ikiendelea kupanua sekta ya usafiri wa anga kupitia ongezeko la ndege mpya, Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kimesema kinaandaa mazungumzo na Serikali ili kuwezesha wanafunzi wanaosomea urubani pamoja na kozi nyingine za anga kupata mikopo ya elimu, hatua inayolenga kuongeza idadi ya wataalamu wa ndani na kupunguza utegemezi wa wataalamu kutoka nje ya nchi.
Mkuu wa NIT, Dkt. Prosper Mgaya, amesema gharama za mafunzo ya urubani na taaluma nyingine za anga bado ni kubwa kwa Watanzania wengi, jambo linalowazuia vijana wenye sifa na uwezo kujiunga na masomo hayo. Amesema upatikanaji wa mikopo utatoa nafasi kwa vijana wengi zaidi kufikia ndoto zao na kuchangia maendeleo ya sekta hiyo.
Kwa mujibu wa Dkt. Mgaya, tafiti zilizofanywa kwa kushirikiana na Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) zimeonyesha kuwa Tanzania bado ina upungufu mkubwa wa marubani, hali inayolazimisha waajiri kutegemea wataalamu kutoka nje ya nchi.
Amesema NIT imejipanga kuwa sehemu ya suluhisho kwa kuongeza uwezo wa kuzalisha wataalamu wa anga watakaokidhi mahitaji ya soko la ajira linaloendelea kukua.
"Mahitaji ya marubani yanaongezeka kadri sekta ya anga inavyopanuka. Lengo letu ni kuhakikisha Watanzania wanapata nafasi ya kusomea taaluma hizi bila kuzuiwa na gharama kubwa za mafunzo," alisema Dkt. Mgaya.
Amefafanua kuwa uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika sekta ya usafiri wa anga, ikiwemo ununuzi wa ndege 16 za kisasa, umeongeza hitaji la marubani na wataalamu wengine wa anga wenye ujuzi wa hali ya juu.
Amesema ndege hizo zinahitaji kuendeshwa na wataalamu wa kutosha kila wakati, hivyo bila kuongeza idadi ya marubani wa ndani, taasisi kama ATCL zitaendelea kutegemea wataalamu kutoka nje, jambo linaloongeza gharama za uendeshaji.
Kutokana na hali hiyo, NIT inatarajia kuwasilisha hoja kwa Serikali ili wanafunzi wanaosomea urubani na fani nyingine za anga wanufaike na mfumo wa mikopo ya elimu, hatua itakayopanua fursa za masomo na kuongeza idadi ya wataalamu wa Kitanzania katika sekta hiyo.
Mbali na mpango huo, Dkt. Mgaya alisema chuo hicho kimeendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia na kupunguza ada katika baadhi ya kozi kwa takribani asilimia 50, huku kikiongeza uwekezaji katika vifaa na ubora wa mafunzo.
Amebainisha kuwa NIT tayari imezalisha wataalamu wengi katika sekta ya usafirishaji, wakiwemo zaidi ya wahandisi na mafundi wa ndege 100 pamoja na wahudumu wa ndege zaidi ya 23, ambao wanaendelea kuhudumu katika taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi.
Pia amesema ushiriki wa wanawake katika taaluma ya urubani unaongezeka kwa kasi, huku idadi yao ikielekea kufikia uwiano unaokaribiana na ule wa wanaume, jambo linaloashiria kuongezeka kwa ushiriki wa wanawake katika taaluma ambazo kwa muda mrefu zilionekana kutawaliwa na wanaume.
Dkt. Mgaya amesisitiza kuwa kuongeza idadi ya wataalamu wa ndani katika sekta ya anga kutaimarisha usalama wa usafiri wa anga, kupunguza gharama za kuajiri wataalamu kutoka nje na kuiwezesha Tanzania kujenga uwezo wake wa kitaalamu kadri sekta hiyo inavyoendelea kukua.






Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...