MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi ya chama cha mapinduzi (CCM) Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro, Mwalimu Meijo Laizer, amempongeza Mkuu wa Mkoa wa zamani, Aggrey Mwanri kufuatia uteuzi wake, wa Naibu katibu mkuu wa chama hicho Bara.
Amesema uongozi wa kweli haupatikani kwa bahati bali hujengwa kupitia uaminifu, nidhamu, uvumilivu na utumishi wa muda mrefu.
Laizer ametoa pongezi hizo kupitia ujumbe alioupa jina la "Kalamu ya Maridhiano", akieleza kuwa, uteuzi wa Mwanri unadhihirisha kuwa kazi njema na rekodi bora za utumishi huzungumza kwa nguvu kuliko maneno akisema hakuna anayeweza kuzuia Mungu kumuinua mtu aliyeandaliwa kwa wakati wake.
Amesema historia huandikwa na viongozi wanaotumikia kwa uadilifu na si kwa makelele, akisisitiza kuwa Mwanri ameandika ukurasa mpya wa heshima ndani ya CCM kutokana na utendaji wake.
Ameongeza kuwa cheo kinaweza kutolewa kwa kalamu, lakini heshima ya uongozi hujengwa kwa matendo, ndiyo maana uteuzi wake umepokelewa kwa furaha na heshima kubwa.
Laizer amesema CCM imeendelea kuthibitisha kuwa huwatambua viongozi wanaoweka mbele maslahi ya Chama na Taifa, akibainisha kuwa Siha imeendelea kuwa eneo linalozalisha viongozi wenye busara, hekima na uzalendo.
Aidha amesema mafanikio ya Mwanri ni motisha kwa vijana na ushahidi kwamba uaminifu, kujituma na nidhamu bado vina thamani katika uongozi.
Akihitimisha ujumbe wake, Laizer amemtakia Mwanri mafanikio katika majukumu yake mapya na kumtaka aendelee kuwa mfano wa uongozi bora.
"Hongera Mheshimiwa Aggrey Mwanri. Endelea kuwa taa ya uongozi, nguzo ya Chama na mfano wa uzalendo kwa vizazi vijavyo. Songa mbele kwa ujasiri mkubwa."amesema Laizer.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...