Makamu Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini anayesimamia Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi, Profesa Provident Jonas Dimoso, amewataka wananchi kujifunza na kutumia fursa zinazotokana na teknolojia za kisasa katika upimaji na usimamizi wa ardhi.

Prof. Dimoso ametoa kauli hiyo wakati Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kikishiriki Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu inayoendelea mkoani Tanga, ambapo chuo hicho kinatoa elimu kuhusu kozi, tafiti na huduma za ushauri elekezi kinazotoa kwa jamii.

Amesema elimu, ujuzi na ubunifu ni nyenzo muhimu katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050, akieleza kuwa chuo hicho kinaendelea kuwekeza katika kuwaandaa wataalamu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya sasa katika sekta ya ardhi na maendeleo.

Prof. Dimoso amesema moja ya maeneo yanayotolewa elimu katika maonesho hayo ni Geomatics, fani inayochanganya maarifa ya Jiografia na Hisabati katika ukusanyaji, uchambuzi na matumizi ya taarifa za ardhi.

Amesema wanafunzi wanaosomea Geomatics hufundishwa kutumia teknolojia na vifaa vya kisasa katika upimaji wa ardhi, ujuzi ambao umewawezesha kushiriki katika shughuli za upimaji katika Halmashauri mbalimbali nchini.

Kwa mujibu wa Prof. Dimoso, wataalamu hao wamekuwa na mchango katika kusaidia kutatua migogoro ya ardhi kupitia upimaji sahihi, hatua inayosaidia kuweka matumizi bora ya ardhi na kuchochea maendeleo katika maeneo mbalimbali.

Amesema kozi ya Geomatics inatolewa katika ngazi za cheti na diploma, huku akieleza kuwa wanafunzi wanaosoma kozi za upimaji ardhi katika ngazi hizo wanapata fursa ya mikopo ya elimu kutoka serikalini.

Prof. Dimoso amewataka wananchi kutumia fursa ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu kutembelea banda la Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini ili kupata elimu kuhusu kozi zinazotolewa, tafiti zinazofanywa pamoja na huduma za ushauri elekezi zinazotolewa na wataalamu wa chuo hicho.

Amesema upatikanaji wa ujuzi wa kisasa katika teknolojia ya upimaji ardhi ni muhimu katika kuimarisha usimamizi wa ardhi, kupunguza migogoro na kuhakikisha ardhi inatumika kwa tija kwa ajili ya maendeleo ya wananchi na taifa.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...