Na Janeth Raphael - MichuziTv
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa kulinda amani na utulivu wa nchi ni hatua muhimu ya kuhakikisha uwekezaji unaendelea kukua, ajira zinapatikana na uchumi unaimarika.
Akizungumza katika Mkutano Maalum wa Serikali na Sekta Binafsi kuhusu utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 uliofanyika Ikulu, Dar es Salaam, Rais Samia alisema maendeleo hayawezi kupatikana bila mazingira salama yanayowapa wawekezaji na wafanyabiashara uhakika wa kufanya shughuli zao.
Ameitaka sekta binafsi kuongeza uwekezaji, uzalishaji, matumizi ya teknolojia na ubunifu, huku ikiwapa nafasi vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na mnyororo wa thamani. Pia amesisitiza umuhimu wa kuongeza thamani ya mazao, kuzingatia viwango vya ubora na kupanua biashara katika masoko ya Afrika na duniani.
Katika mkutano huo, Rais Samia alizindua nyenzo za utekelezaji wa Dira 2050 na kukabidhi Ufunguo wa Mtazamo Mpya unaoashiria mwanzo wa ushirikiano mpya kati ya Serikali na sekta binafsi. Aidha, aliiagiza Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji kuhakikisha wadau wote wanafahamu nyenzo hizo ili kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa dira hiyo.
Kwa upande wake, Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, aliahidi ushirikiano wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutekeleza Dira 2050, akieleza kuwa maeneo ya uwekezaji, sayansi, teknolojia, uchumi wa kidijitali, uchumi wa buluu na maendeleo ya rasilimali watu yatapewa kipaumbele.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, alisema maboresho ya mazingira ya biashara yameongeza imani ya wawekezaji na kuifanya Tanzania kuvutia zaidi mitaji, huku Rais wa Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Angelina Ngalula, akipongeza hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kuboresha sera, sheria na mifumo ya uwekezaji.
Wawakilishi wa sekta binafsi waliihakikishia Serikali kuendelea kushirikiana katika kuongeza uwekezaji, teknolojia na ajira, huku wakisisitiza umuhimu wa sera zinazotabirika na mashauriano ya mara kwa mara kuhusu mazingira ya biashara.
Katika hafla hiyo, Rais Samia pia alishuhudia utiaji saini wa Tamko la Pamoja kati ya Serikali na Sekta Binafsi kuhusu utekelezaji wa Dira 2050, kabla ya kutunukiwa Tuzo ya Heshima kutoka sekta binafsi kwa mchango wake katika kuboresha mazingira ya biashara, uwekezaji na kukuza uchumi shirikishi nchini.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akipokea Tuzo ya Heshima kutoka Rais wa Chemba ya Taifa ya Biashara Tanzania (TNCC), Bw. Vicent Minja katika hafla ya uzinduzi wa Nyenzo za Utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 03 Agosti, 2026.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi mbalimbali kabla ya kuzindua Nyenzo za Utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 03 Agosti, 2026.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwakabidhi mfano wa Ufunguo kama ishara ya mtazamo mpya, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo, Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar, Dkt. Juma Malick Akil, Rais wa Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) Bi. Angelina Ngalula pamoja na Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara Zanzibar (ZNCC), Bw. Ali Amour baada ya uzinduzi Nyenzo za Utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 03 Agosti, 2026.



.jpeg)

.jpeg)



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...