Na: Calvin Gwabara – Dodoma.

Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) imeeleza kuwa imefanikiwa kuokoa zaidi ya tani milioni 2.1 za chakula msimu uliopita na ekari zaidi ya 700,000 baada ya kudhibiti milipuko ya visumbufu vya mazao, ikiwemo ndege aina ya Kwelea kwelea, Panya na Viwavi Jeshi.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. James Kinyasi Millya (Kulia) akimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA Prof. Joseph Ndunguru

Akizungumza jijini Dodoma kwenye maonesho ya wakulim Nanenane kitaifa, Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Prof. Joseph Ndunguru, amesema mamlaka hiyo ina mchango mkubwa katika kuhakikisha Tanzania inafikia utoshelevu wa chakula unaofikia asilimia 130, kupitia udhibiti wa wadudu, magonjwa ya mimea na visumbufu mbalimbali vinavyohatarisha uzalishaji wa mazao.

Amesema katika msimu uliopita, TPHPA ilidhibiti uvamizi wa ndege aina ya kwelea kwelea wapatao milioni 231 waliovamia skimu kubwa za mpunga, hususan maeneo ya Mbarali Mkoani Mbeya, Bariadi Mkoani Simiyu na Kilosa Mkoani Morogoro, hatua iliyosaidia kuokoa zaidi ya tani milioni 1.6 za chakula.

“Kwa mfano, tunadhibiti visumbufu milipuko kama vile ndege aina ya Quelea quelea, ambao wanaharibu nafaka kwa kula mpunga, mtama na uwele. Msimu uliopita tulikuwa na uvamizi wa ndege hao wapatao milioni 231 katika skimu kubwa za mpunga. Tulienda kuwazuia kwa kutumia ndege maalum na tuliweza kuokoa zaidi ya tani milioni 1.6 za chakula,” amesema Prof. Ndunguru.

Aidha, amesema mamlaka hiyo ilidhibiti uvamizi wa panya katika mikoa 19 na wilaya 54, ambapo hatua zilizochukuliwa ziliwezesha kuokoa takribani ekari 408,000 za mazao huku kwa upande wa viwavi jeshi vamizi waliokoa zaidi ya ekari 219,000, ambapo udhibiti wake uliwezesha kuokoa tani 519,000 za mahindi.

Amesema jitihada hizo zimechangia kuongeza uzalishaji wa mahindi nchini na kuipandisha Tanzania kutoka nafasi ya tatu hadi ya pili kwa uzalishaji wa mahindi barani Afrika, ikitanguliwa na Afrika Kusini.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. James Kinyasi Millya, ameipongeza TPHPA kwa juhudi zake za kuhakikisha wakulima wanapata masoko ya uhakika kwa mazao yao kwani uzalishaji mkubwa bila soko kunaweza kuwakatisha tamaa wakulima.

Amesema Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki iko tayari kushirikiana na TPHPA katika kutafuta masoko ya mazao ya Tanzania kupitia balozi za nchi hiyo zilizopo katika mataifa mbalimbali duniani.

“Jambo kubwa ambalo nimelifurahia ni jinsi mnavyopambana kutafuta masoko ya wakulima wetu. Tunahimiza kuzalisha sana, lakini mwisho wakikosa masoko na kupata hasara wanaweza kukata tamaa. Hivyo, nyinyi mnatusaidia sana kwa upande wa Serikali kuondoa changamoto hiyo,” amesema Mhe. Millya.

Amesema ushirikiano huo ni sehemu ya maagizo maalumu ya Rais kwa mabalozi wa Tanzania kushirikiana na taasisi zinazohusika na uzalishaji na biashara ya mazao ili kuwezesha bidhaa za wakulima wa Tanzania kupata masoko katika nchi wanazowakilisha.

Mhe. Millya ameitaka TPHPA kutumia fursa zilizopo katika masoko ya kimataifa, akitolea mfano zao la ndizi zinazozalishwa Bukoba na kupelekwa katika baadhi ya masoko ya nje, ikiwemo Marekani na Canada.

“Naomba TPHPA iangalie fursa ya zao la ndizi za Bukoba zinazokwenda Marekani, Canada na nchi nyingine, shirikianeni na balozi zetu kuona namna gani tunaweza kupeleka ndizi zetu katika nchi hizo na kuongeza masoko kwa wakulima wetu,” amesema Mhe. Millya.

Amesema ushirikiano kati ya TPHPA na Wizara ya Mambo ya Nje ni muhimu katika kuhakikisha mazao ya Tanzania yanapata masoko ya uhakika nje ya nchi, huku akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wakulima na wadau wa sekta ya kilimo kuongeza uzalishaji na tija. 


MATUKIO KATIKA PICHA KWENYE BANDA LA TPHPA 





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...