📌 Ni katika mkakati wa kuokoa hekta 470,000 za misitu zinazoteketea kila mwaka kote nchini
Busega, Simiyu📍
WAKALA wa Nishati Vijijini (REA) imegawa majiko ya gesi ya mtungi wa kilo sita kwa wananchi 150 wa Wilaya ya Busega mkoani Simiyu, ikiwa ni sehemu ya kuongeza kasi ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024–2034).
Ugawaji huo ulifanyika Jualia 31, 2026, katika hafla iliyoenda sambamba na kilele cha ufungaji wa Mbio za Mwenge Kitaifa mkoani humo. Hafla hiyo iliongozwa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Bw. Wazo Michael Mwang’onda, na kushuhudiwa na Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe. Faidha Salim, pamoja na Mbunge wa Jimbo la Busega, Mhe. Simon Songe.
Akizungumza wakati wa ugawaji huo, Bw. Mwang’onda aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi. Alibainisha kuwa juhudi hizo zitasaidia kufikia lengo la asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati mbadala ifikapo mwaka 2034.
"Nawapongeza REA kwa kutekeleza kwa vitendo mkakati huu. Juhudi hizi ni za kuungwa mkono na kila mdau ili kulinda mazingira na afya za wananchi wetu," alisema Bw. Mwang’onda.
Mmoja wa wanufaika wa mradi huo, Bi. Jane Samson, ambaye ni Mama Lishe kutoka Kitongoji cha Chamgasa, Kijiji cha Kalemela, aliishukuru REA na kueleza kuwa majiko hayo yatapunguza adha ya kupika kwa kutumia kuni na mkaa ambayo ni ya gharama kubwa na inasumbua, hasa nyakati za masika.
Utekelezaji wa mradi huu unakuja wakati takwimu za mazingira zikionyesha kuwa Tanzania inapoteza kati ya hekta 370,000 hadi 470,000 za misitu kila mwaka kutokana na uvunaji wa kuni na mkaa. Zaidi ya asilimia 90 ya kaya na taasisi nchini bado zinategemea nishati hiyo ya asili, hali inayochangia pia magonjwa ya mfumo wa upumuaji na matatizo ya macho kutokana na moshi wenye gesi sumu ya ukaa (Carbon Monoxide).


.jpeg)




Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...