WANAFUNZI 34 waliochaguliwa kupitia mpango wa ufadhili wa Samia Scholarship Extended wameondoka nchini leo Agosti 28, 2026 kuelekea Ireland kwa ajili ya kuanza masomo ya shahada katika fani za Sayansi ya Data, Akili Unde na Sayansi Shirikishi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuandaa wataalamu wa sayansi na teknolojia.
Akizungumza wakati wa kuwaaga wanafunzi hao, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Siylvia Lupembe amesema kundi hilo ni sehemu ya wanafunzi 50 waliochaguliwa kwenda kusoma katika vyuo bora duniani, ambapo wanafunzi 16 tayari wamekwenda Afrika Kusini na wanafunzi 34 waliobaki ndo wameondoka leo kwenda Ireland.
Lupembe amesema wanafunzi hao watasoma katika vyuo viwili nchini Ireland, kikiwemo Chuo Kikuu cha Limerick, na kwamba mbali na masomo ya darasani, watapata pia fursa ya kufanya mafunzo kwa vitendo katika kampuni kubwa za teknolojia.
"Leo hawa ambao tunawaaga hapa uwanja wa ndege ni 34. Wanaenda Ireland na watasoma katika vyuo viwili, masomo hayo hayo ya Sayansi ya Data, Akili Unde na Sayansi Shirikishi, pamoja na mafunzo mengine yanayohusiana na teknolojia,” amesema.

Amesema Serikali imechagua vyuo hivyo kutokana na uwezo wake wa kutoa elimu katika maeneo hayo pamoja na kuwa na ushirikiano na kampuni kubwa za teknolojia, hatua itakayowawezesha wanafunzi kupata uzoefu wa vitendo kabla ya kurejea nchini.
Ameongeza kuwa mpango huo ni endelevu na Serikali tayari imepata nafasi nyingine ya kuwapeleka wanafunzi 10 kusoma nchini Urusi, huku akisisitiza kuwa wataalamu hao wanatarajiwa kuwa chachu ya mabadiliko katika sekta mbalimbali nchini.

Akieleza zaidi kuhusu programu hiyo, Profesa, Steven Maruka amesema wanafunzi hao wamepata ufadhili kupitia mpango wa Samia Scholarship Extended, baada ya kufanya vizuri zaidi katika matokeo ya Kidato cha Sita.
Amesema kabla ya kuanza masomo ya shahada ya kwanza, wanafunzi hao walipitia mafunzo maalumu ya maandalizi kwa kipindi cha takribani miezi 10 ili kuwaandaa kukabiliana na masomo wanayokwenda kusomea.
“Wanaenda kusoma masuala yanayohusiana na Sayansi ya Data, Akili Unde na Sayansi Shirikishi. Hawa ni wanafunzi ambao walikuwa na ufaulu wa juu kuliko wote katika matokeo ya Kidato cha Sita,” amesema.
Profesa huyo amesema kuanzia mwaka wa masomo 2026, Serikali imepanua wigo wa programu hiyo kwa kuanza kufadhili wanafunzi wenye ufaulu wa juu kwenda kusoma nje ya nchi, ikiwa ni mara ya kwanza kwa mpango huo kuwapeleka wanafunzi hao katika vyuo vya nje.

Mwanafunzi: Tumepewa fursa ya kutimiza ndoto
Mmoja wa wanafunzi hao, Angela Mombi, amesema anashukuru Serikali kwa kumpa nafasi ya kuendelea na masomo ya shahada ya kwanza nchini Ireland kupitia mpango huo.
Angela amesema amepata nafasi ya kusoma Shahada ya Sayansi katika chuo kilichopo Ireland, baada ya kumaliza Kidato cha Sita katika Shule ya St. Mary's Mazinde Juu, Tanga.
Amesema fursa hiyo kwake ni hatua kubwa katika kutimiza ndoto zake za kielimu, huku akiahidi kusoma kwa bidii na kutumia elimu atakayoipata kwa manufaa ya Tanzania.

Kwa upande wake, mzazi wa mwanafunzi Sangalu Mahinuka aliyepata fursa hiyo ya kwenda kusoma nje ya nchi, kutoka mkoani Simiyu, Mbogolo Kushaha ameishukuru Serikali kwa kutoa fursa hiyo, akisema inalenga kuandaa wataalamu katika eneo la teknolojia ambalo linaendelea kukua kwa kasi duniani.
Amesema wanafunzi hao wanapaswa kutumia fursa hiyo kujifunza kwa bidii ili watakaporejea nchini waweze kutumia ujuzi na teknolojia watakazozipata katika kutatua changamoto mbalimbali.
Mzazi huyo amewataka wazazi wengine nchini kuwahamasisha watoto wao kusoma kwa bidii ili waweze kutumia fursa za ufadhili zinazotolewa na Serikali na hatimaye kupata ujuzi utakaosaidia maendeleo ya taifa.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...