Na Janeth Raphael - MichuziTv - Bungeni


Serikali imesema haina mpango wa kuunda Tume maalum ya Taifa ya kutatua migogoro ya ardhi nchini, badala yake imeandaa Mkakati wa Kudumu wa Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi Nchini utakaotumika na taasisi mbalimbali za Serikali katika kushughulikia migogoro hiyo.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Kaspare Mmuya, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Asha Ramadhani Baraka, aliyetaka kujua lini Serikali itaunda Tume itakayokuwa na jukumu la kutatua migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali nchini.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Mmuya amesema Serikali imeona umuhimu wa kutumia mfumo wa pamoja unaowezesha taasisi zinazohusika kushughulikia migogoro ya ardhi kwa utaratibu unaofanana, badala ya kuanzisha Tume nyingine.

Amesema Mkakati huo utaiwezesha Serikali kuwa na kanzidata moja inayohifadhi taarifa za migogoro ya ardhi nchini, hatua itakayosaidia kuondoa changamoto ya mgogoro mmoja kushughulikiwa na taasisi zaidi ya moja na hatimaye kutolewa kwa maamuzi yanayotofautiana.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri, mfumo huo utasaidia kuongeza uelewa, uwazi na uwajibikaji miongoni mwa taasisi zinazohusika, huku ukiongeza kasi ya kushughulikia na kutatua migogoro ya ardhi.

Amesema Serikali inalenga kupitia mkakati huo kuimarisha amani, umoja na mshikamano katika jamii, sambamba na kuboresha mazingira ya uwekezaji katika ardhi na kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi.

Naibu Waziri Mmuya amesema kwa sasa Mkakati wa Kudumu wa Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi Nchini upo katika hatua za ukamilishaji na mara utakapokamilika utaanza kutumiwa na taasisi zote husika.

Hatua hiyo inatarajiwa kuweka mfumo mmoja wa kitaifa wa kushughulikia migogoro ya ardhi, kwa kuimarisha uratibu wa taasisi za Serikali na kuhakikisha migogoro inashughulikiwa kwa ufanisi, uwazi na kwa maamuzi yanayokwenda sambamba.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...