Na Belinda Joseph- Dodoma
Mratibu wa Mtandao wa Mashirika Yanayojishughulisha na Utunzaji wa Bionuai Tanzania (TABIO), Abdallah Ramadhan Mkindi, amesema taasisi hiyo inaendelea kuhamasisha uhifadhi na matumizi ya mbegu za asili pamoja na mifugo ya asili, ikiwemo ng’ombe na kuku wa kienyeji, ili isipotee kutokana na mchango wake mkubwa katika usalama wa chakula na uhifadhi wa mazingira nchini.
Mkindi ameyasema hayo Agosti 5, 2026, jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mkutano wa wadau wa kilimo ikolojia uliofanyika katika Maonesho ya Kilimo ya Nanenane Kitaifa.
Amesema mkutano huo umejikita kujadili namna ya kuendelea kutunza mbegu za asili, kuongeza matumizi yake katika uzalishaji wa chakula, pamoja na kuhamasisha mamlaka husika kuzitambua na kuzipa msaada ili ziendelee kukua na kutoa mchango mkubwa katika kuimarisha usalama wa chakula nchini na duniani kwa ujumla.
Aidha, amesema wadau hao wamejadili matumizi ya pembejeo za kilimo hai, ikiwemo viuatilifu vya kudhibiti visumbufu vya mimea na mbolea rafiki kwa mazingira ambazo haziachi mabaki yenye madhara kwa afya ya binadamu baada ya kutumika katika uzalishaji wa mazao.
Mkindi amesema pia wanatambua kuwa wakulima wanahitaji masoko ya uhakika kwa mazao yao, kwa kuwa kilimo ni chanzo kikuu cha kipato na chakula kwa familia nyingi, amesema wakulima wanaozalisha kwa kutumia mbinu za kilimo ikolojia huzalisha mazao mbalimbali, ikiwemo mahindi ya rangi tofauti kama njano, buluu, mekundu na yenye mchanganyiko wa rangi, ambayo yana virutubisho vingi.
Hata hivyo, amesema baadhi ya mamlaka zilizopewa jukumu la kununua nafaka bado hazinunui mahindi hayo kutokana na rangi zake, jambo ambalo linawakosesha wakulima soko licha ya thamani kubwa ya lishe iliyopo kwenye mazao hayo.
Kutokana na hali hiyo, amesema mkutano huo umejadili namna ya kushawishi mamlaka zinazohusika na ununuzi wa mazao kuingiza mahindi hayo katika mfumo rasmi wa ununuzi, sambamba na kuboresha huduma za ugani ili wakulima wapate taarifa sahihi zitakazowawezesha kuongeza tija katika shughuli zao za kilimo.
Kwa upande wake, Mratibu wa Utafiti na Masuala ya Kisera kutoka taasisi ya Swiz Aid Tanzania, Gladness Martine, amesema taasisi hiyo imeshiriki mkutano huo kwa lengo la kushirikisha uzoefu wake kuhusu umuhimu wa tafiti shirikishi katika kuwasaidia wakulima kuhifadhi, kulinda na kuendeleza matumizi ya mbegu za asili kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.




Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...