Na Janeth Raphael -MichuziTv


Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limewataka wafugaji nchini kuachana na tabia ya kutumia dawa za mifugo bila ushauri wa wataalamu wa afya ya wanyama, likionya kuwa matumizi yasiyo sahihi ya dawa hizo yanachochea kuongezeka kwa usugu wa vimelea dhidi ya dawa (Antimicrobial Resistance – AMR), tatizo linalotishia afya ya mifugo, binadamu na usalama wa chakula.

Tahadhari hiyo imetolewa na Mratibu wa Mradi wa Kudhibiti Usugu wa Vimelea dhidi ya Dawa (AMR) wa FAO, Elibariki Mwakapeje, wakati akizungumza na wafugaji na wadau wa sekta ya mifugo katika Maonesho ya 31 ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma.

Mwakapeje amesema kuwa matumizi ya dawa za mifugo bila ushauri wa wataalamu yameendelea kuwa changamoto inayochangia kupungua kwa uwezo wa dawa kutibu magonjwa mbalimbali ya mifugo, hali inayoweza kusababisha hasara kubwa katika uzalishaji na kuhatarisha afya ya jamii kwa ujumla.

Amefanua kuwa FAO imeamua kutumia jukwaa la Maonesho ya Nanenane kufikisha elimu kwa wafugaji kuhusu matumizi sahihi ya dawa za mifugo, ikiwahamasisha kuhakikisha dawa zinatumika pale tu zinapohitajika na kwa kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya ya wanyama.

"Lengo letu ni kuhakikisha wafugaji wanaelewa umuhimu wa kutumia dawa za mifugo kwa usahihi na kutambua madhara makubwa yanayotokana na matumizi holela ya dawa hizo," alisema Mwakapeje.

Amesisitiza kuwa wafugaji wanapaswa kuepuka tabia ya kujinunulia dawa na kuwatibu wanyama bila ushauri wa kitaalamu, akieleza kuwa kufanya hivyo kunaongeza hatari ya kuibuka kwa vimelea vinavyoshindwa kutibika kwa dawa zilizopo.

Kwa mujibu wa Mwakapeje, usugu wa vimelea dhidi ya dawa ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazoongezeka duniani, kwani unapunguza ufanisi wa dawa zinazotumika kutibu na kudhibiti magonjwa ya mifugo. Matokeo yake ni kuongezeka kwa gharama za uzalishaji, kupungua kwa tija na kuhatarisha upatikanaji wa chakula salama kwa walaji.

Mbali na matumizi sahihi ya dawa, Mwakapeje aliwahimiza wafugaji kuzingatia kanuni bora za usafi katika ufugaji ikiwemo kusafisha mabanda mara kwa mara, kuhakikisha vyombo vya kunyweshea maji na kulishia mifugo vinakuwa safi pamoja na kuimarisha mazingira ya ufugaji.

Amesema hatua hizo ni muhimu katika kuzuia magonjwa kabla hayajatokea, hivyo kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ya dawa za mifugo.


"Afya bora ya mifugo inaanzia kwenye kinga. Wafugaji wanapowekeza katika usafi na biosecurity, wanapunguza kwa kiwango kikubwa uwezekano wa magonjwa na matumizi ya dawa," alieleza.

Aidha, amesema matumizi holela na ya kupita kiasi ya dawa za mifugo yanaweza kuwa na athari zinazovuka sekta ya mifugo pekee, kwani yanaweza kuhatarisha afya ya binadamu kupitia mnyororo wa chakula pamoja na kuathiri mazingira.

Kutokana na hali hiyo, alisisitiza kuwa mapambano dhidi ya usugu wa vimelea yanahitaji ushirikiano wa karibu kati ya wafugaji, madaktari wa mifugo, wataalamu wa afya, taasisi za utafiti, serikali na wadau wote wa mnyororo wa thamani wa chakula.

Mwakapeje amebainisha kuwa FAO itaendelea kutumia majukwaa mbalimbali ya elimu ya umma, ikiwemo Maonesho ya Nanenane, kuongeza uelewa kuhusu matumizi salama na yenye uwajibikaji ya dawa za mifugo ili kulinda afya ya wanyama, afya ya binadamu na kuhakikisha upatikanaji wa chakula salama.

Amehitimisha kwa kuwakumbusha wafugaji kuwa kaulimbiu ya "Kinga ni Bora Kuliko Tiba" ndiyo msingi wa ufugaji wenye tija na endelevu, akisisitiza kuwa kuzuia magonjwa kupitia usafi, lishe bora na usimamizi sahihi wa mifugo ni njia bora zaidi kuliko kutegemea matumizi ya dawa baada ya magonjwa kutokea.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...