Na Mwandishi Wetu

UMOJA wa Wahitimu wa Shule ya Sekondari Tosa Maganga (TAO) umeanzisha kampeni ya kuchangisha Sh milioni 250 kwa ajili ya ununuzi wa basi jipya la shule hiyo, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya miaka 100 tangu kuanzishwa kwake.

Aidha, imewataka wahitimu wote wa Tosa Maganga na wadau mbalimbali kushirikiana katika kufanikisha ununuzi wa basi hilo, wakisisitiza kuwa mchango wa kila mmoja ni muhimu katika kutimiza azma hiyo.

Hayo yalisema leo jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa kamati ndogo ya ununuzi wa basi hilo, Iddy Mwerangi, ambaye ni alumnus wa mwaka 1996–1998, alisema TAO imeamua kubeba jukumu hilo ili kuiwezesha shule kupata usafiri wake wa kudumu na kupunguza gharama zinazotumika kukodi magari kwa shughuli mbalimbali.

Alisema basi hilo linalotarajiwa kununuliwa ni aina ya Yutong D14, ambalo litakuwa na uwezo wa kubeba abiria 77, litatumika katika safari za kitaaluma, michezo, shughuli za kijamii pamoja na dharura, huku akieleza kuwa ununuzi wa basi hilo utasaidia kuongeza hadhi ya shule ambayo kwa sasa ni miongoni mwa shule za vipaji maalum.

"TAO tayari imefanya mawasiliano na kampuni ya Yutong nchini China pamoja na wakala wake nchini Tanzania kwa ajili ya kupata maelezo na mahitaji muhimu ya basi hilo,"alisema Mwenyekiti Mwerangi

Kwa mujibu wa Mwerangi, TAO inatarajia kupata fedha hizo kupitia michango kutoka kwa wahitimu wa shule hiyo waliopo ndani na nje ya Tanzania, taasisi, kampuni, wafanyabiashara na watanzania wengine wenye nia ya kuiunga mkono Tosa Maganga.

"Michango yote itapokelewa kupitia akaunti rasmi ya Tosa Maganga Alumni Organization na itaorodheshwa kwa ajili ya kuhakikisha uwazi na uwajibikaji.Kampeni hiyo ni sehemu ya miradi iliyopangwa katika maadhimisho ya miaka 100 ya Tosa Maganga, ambayo yanatarajiwa kufanyika Oktoba 8 hadi 10, 2026, Iringa,"alisema

Alibainisha kuwa kamati ya shule na bodi wameainisha miradi minne, ikiwemo ununuzi wa viti na meza za bwalo la chakula, ukarabati wa mabweni ya Muungano na Madera, pamoja na ununuzi wa basi hilo, TAO imechukua jukumu la kutafuta Sh milioni 250 kwa ajili ya basi, sawa na asilimia 25 ya lengo la jumla la Sh bilioni moja la miradi ya jubilee.

Kwa upande wake, Katibu wa kamati hiyo, Grayon Nyamoga amewataka wahitimu wa shule hiyo kushirikiana katika kuchangisha fedha hizo zitakazotumika kununua basi jipya la shule hiyo.

"Lengo hili linawezekana kutokana na idadi kubwa ya wahitimu waliopo, endapo wahitimu 10,500 watatoa kiwango cha chini cha Sh 50,000 kila mmoja, zaidi ya Sh milioni 500 zinaweza kupatikana, hivyo kuwezesha ununuzi wa basi pamoja na kushiriki katika miradi mingine ya maadhimisho ya miaka 100 ya shule hiyo,"alisema.

Nyamoga alisema TAO imeweka utaratibu wa kuhakikisha fedha zitakazochangwa kwa ajili ya basi zinakuwa salama na zinatumika kwa uwazi, akiwahakikishia alumni kuwa akaunti inayotumika kukusanya michango ni ya taasisi inayotambulika na kusajiliwa.

"Kamati pia imekubaliana kutoa taarifa za makusanyo kwa makundi mbalimbali ya alumni ili kila mhitimu aweze kufuatilia maendeleo ya zoezi hilo na kuwa na imani na matumizi ya fedha zinazokusanywa,"alisema

Aidha, alisema kamati itaendelea kushirikiana na uongozi wa shule, Manispaa pamoja na taasisi na mamlaka husika kuhakikisha mchakato wa ununuzi wa basi unafanyika kwa kuzingatia taratibu zote.
Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Ununuzi wa Basi la Shule la Tosa Maganga, Iddy Mwerangi
Katibu wa kamati Ndogo ya ununuzi wa basi la shule ya Tosa Maganga, Dk Greyson Nyamoga

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...