
Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Ukusanyaji Mapato Tanzania (TAREWU) Wakili na CPA Dkt.Michael Marere na Mkurugenzi Mtendaji wa Global Dynamic Consulting (GDC) Anne Massawe wakisaini hati za makubaliano katika hafla iliyofanyika Ofisi za GDC jijini Dar es Salaam.
.jpeg)
Mkuugenzi wa Mtendaji wa Global Dynamic Consulting Anne Massawe akizungumza namna watavyoshirikiana na TAREWU katika makubaliano ya usimamizi wa miradi ya maendeleo ya uongozi.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Ukusanyaji Mapato Tanzania (TAREWU) Dkt.Michael Marere akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana TAREWU kuingia makubaliano na Global Dynamic Consulting (GDC) kwa ajili ya usimamizi wa miradi ya maendeleo na uongozi.
Baadhi ya matukio katika picha mara baada ya kusaini makubaliano
Na Mwandishi Wetu
CHAMA cha Wafanyakazi Wakusanya Mapato Tanzania (TAREWU) kimesaini Hati ya Makubaliano (MoU) na Global Dynamics Consulting (GDC), kwa lengo la kuimarisha uwezo wa wanachama wake katika usimamizi wa miradi na maendeleo ya uongozi.
Ushirikiano huo unalenga kuwawezesha wafanyakazi na viongozi kupata ujuzi, maarifa na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taasisi zao na taifa kwa ujumla.
Akizungumza mara baada ya kusaini hati hiyo, Katibu Mkuu wa TAREWU, Wakili na CPA Dkt. Michael Marere, amesema ushirikiano huo ni sehemu ya mkakati mpana wa chama wa kuwajengea wanachama uwezo na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya kitaaluma na kiuchumi.
Amesema TAREWU itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha wanachama wanapata fursa za kuongeza ujuzi, kubadilishana uzoefu na kunufaika na programu zinazolenga kuimarisha uwezo wao.
Dkt. Marere amesema makubaliano hayo yatawezesha taasisi hizo mbili kuandaa na kutekeleza programu mbalimbali za mafunzo, semina na shughuli nyingine zinazolenga kuongeza uwezo wa wafanyakazi na viongozi katika maeneo mbalimbali.
Amesema ushirikiano na GDC pia utalenga kuandaa programu za kukuza uongozi wenye ufanisi, kuimarisha uwezo wa viongozi katika taasisi mbalimbali na kuwajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kwa mujibu wa TAREWU, upatikanaji wa viongozi wenye uwezo ni muhimu katika kuhakikisha taasisi zinafanya kazi kwa ufanisi na kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.
Chama hicho kimesema mazingira ya sasa yanahitaji viongozi wenye uwezo wa kufanya maamuzi sahihi, kusimamia rasilimali kwa ufanisi na kuongoza mabadiliko yanayolenga kuboresha utendaji wa taasisi.
Aidha, TAREWU imesisitiza umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika mafunzo na maendeleo ya viongozi ili kuwawezesha kukabiliana na changamoto zinazotokana na mabadiliko ya kijamii, kiuchumi na kiteknolojia.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Global Dynamics Consulting (GDC), Anne Massawe, amesema kampuni hiyo ina dhamira ya kuendelea kusaidia taasisi mbalimbali kuimarisha mifumo bora ya uongozi na kuongeza uwezo wa utekelezaji wa miradi.
Massawe amesema kusainiwa kwa hati hiyo ni hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi hizo, huku akisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika maendeleo ya rasilimali watu kwa manufaa ya wanachama na jamii kwa ujumla.
Chini ya makubaliano hayo, TAREWU na GDC zinatarajia kutekeleza programu za kujenga uwezo katika usimamizi wa miradi na uongozi, warsha na semina za mafunzo, programu za uelekezi na ushauri elekezi kwa wanachama, pamoja na mijadala ya kubadilishana maarifa.
Shughuli nyingine zitakazotekelezwa ni pamoja na kutoa fursa za kujenga mitandao ya kitaalamu, tafiti na ubunifu unaolenga kuongeza uelewa na kuboresha utendaji wa taasisi.
Taasisi hizo zimesema juhudi hizo zinalenga kuhakikisha viongozi wanakuwa na maarifa, ujuzi na mtazamo unaowawezesha kuleta matokeo chanya katika taasisi wanazoziongoza.





Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...