.jpeg)
Na Mwandishi Wetu
CHUO cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi na Huduma VETA Chang’ombe, Dar es Salaam, kimesema mafunzo ya ubunifu wa mavazi na mitindo yanaendelea kuwa chachu ya kuwawezesha vijana kujiajiri, kuajiri wengine na kuchangia katika kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira nchini.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Chuo cha VETA Chang’ombe, Abraham Richard Mbughuni, wakati wa onyesho la kazi za wanafunzi wa mwaka wa tatu wa kozi ya Diploma ya Ubunifu wa Mavazi na Mitindo, ambapo wanafunzi waliwasilisha kazi zao ikiwa ni sehemu ya mtihani wa mwisho.
Mbughuni alisema ubunifu ulioonyeshwa na wanafunzi hao ni kielelezo cha maarifa na ujuzi walioupata chuoni, huku akieleza kuwa unathibitisha jitihada za VETA katika kuzalisha wahitimu wenye uwezo wa kushindana katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.
Alisema Serikali imeendelea kuwekeza katika elimu ya ufundi na stadi kupitia VETA, hatua inayowawezesha vijana kupata ujuzi wa kujitegemea badala ya kutegemea ajira rasmi ambazo mahitaji yake ni makubwa kuliko nafasi zilizopo.
“Kila ubunifu na muundo wa vazi unaoonyeshwa ni msingi wa ajira za baadaye na unaweza kuwa nembo ya Tanzania katika sekta ya ubunifu. Wanafunzi hawa si wahitimu pekee, bali ni wajasiriamali na waajiri wa kesho,” alisema.
Mbughuni aliwataka wadau mbalimbali kuendelea kuunga mkono sekta ya ubunifu wa mavazi kwa kuweka mazingira bora yatakayowezesha sekta hiyo kukua.
Alisema iwapo vyuo vya VETA vitaendelea kuzalisha wabunifu wengi kila mwaka, Tanzania itaongeza uwezo wa kuzalisha mavazi yake yenyewe na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Textile and Fashion Design katika VETA Dar es Salaam, Josephat Maghina, alisema onyesho hilo lilikuwa sehemu ya mtihani wa mwisho wa wanafunzi, ambapo kila mwanafunzi alitakiwa kuandaa mkusanyiko wa mavazi matano yaliyobuniwa kutokana na wazo au msukumo aliouchagua.
Maghina alisema mafunzo ya sasa yanazingatia ubunifu wa kisasa unaoanzia katika utafiti, uchoraji wa michoro, maandalizi ya kazi hadi utengenezaji wa mavazi, tofauti na mtazamo wa zamani wa kushona bila kufuata mchakato wa kitaalamu.
Alisema kozi hiyo inawawezesha wahitimu kujiajiri, kuajiriwa katika taasisi mbalimbali na kuanzisha biashara zao, huku akiwahimiza vijana wenye sifa kujiunga na VETA ili kunufaika na fursa zinazopatikana katika sekta ya mitindo na mavazi.
“Mahitaji ya wabunifu wa mavazi yanaendelea kuongezeka kutokana na ukuaji wa tasnia hii. Wahitimu wetu wana uwezo wa kushiriki katika matukio makubwa ya kitaifa na kimataifa, ikiwemo kubuni mavazi kwa viongozi na mashindano mbalimbali,” alisema Maghina.
Mhitimu wa kozi hiyo, Andrea Johannes, alisema mafunzo aliyoyapata yamemjengea uwezo wa kuingia kwa kujiamini katika soko la ajira, akieleza kuwa lengo lake ni kujiajiri na baadaye kuajiri vijana wengine baada ya kuanzisha karakana yake ya ushonaji.
Naye mhitimu, Beatrice Richard Mahimbo, alisema ujuzi walioupata kutoka kwa wakufunzi wa VETA umewapa msingi wa kujitegemea kiuchumi, huku akiahidi kuwahamasisha vijana wengine kujiunga na kozi hiyo ili kuongeza idadi ya wabunifu wenye uwezo nchini.
Jumla ya wanafunzi 27 wamehitimu mafunzo ya Diploma ya Ubunifu wa Mavazi na Mitindo, huku uongozi wa chuo ukieleza kuwa una imani wahitimu hao watakuwa sehemu ya nguvu kazi itakayochochea maendeleo ya sekta ya mitindo, kuongeza ajira na kuunga mkono juhudi za Tanzania za kujenga tasnia imara ya mavazi




.jpeg)




Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...