Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imesema Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo na Ufugaji Nane Nane ni muhimu katika kutoa elimu kwa wakulima na wafugaji kuhusu matumizi sahihi ya dawa za kilimo na mifugo.
Akizungumza katika Maonesho hayo yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Samwel Malecela jijini Dodoma, Mkaguzi wa Dawa wa TMDA, Benedict Brashi, amesema matumizi yasiyo sahihi ya dawa za kilimo na mifugo yanaweza kusababisha madhara kwa afya ya binadamu na mazingira.
Amesema dawa zinazotumika katika kilimo na ufugaji zinahitaji kuzingatia ushauri wa wataalamu pamoja na muda wa kusubiri baada ya matumizi, kabla ya mazao au bidhaa za mifugo kuanza kutumika au kuuzwa.
“Dawa zikitumika katika kilimo au ufugaji, ni muhimu kuzingatia ushauri wa wataalamu kwa muda wanaopewa ili Mazao au nyama vikiingizwa sokoni visiwe na madhara kwa afya ya mlaji,” amesema Brashi.
Aidha, amesema ulinzi dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na matumizi yasiyo sahihi ya dawa ni jukumu la kila mwananchi, huku akiwataka wananchi kutoa taarifa pindi wanapobaini matumizi yasiyo sahihi ya dawa ili hatua stahiki zichukuliwe.
Brashi pia amesisitiza kuwa dawa za kilimo, mifugo na binadamu zilizomaliza muda wake hazipaswi kutupwa kiholela, kwa kuwa zinaweza kusababisha madhara kwa afya ya binadamu na mazingira.
Amesema dawa hizo zinapaswa kupelekwa katika hospitali, vituo vya afya au zahanati kwa ajili ya kushughulikiwa na kuteketezwa kwa utaratibu unaostahili.
Amesema TMDA inaendelea kutumia maonesho hayo kuwaelimisha wananchi kuhusu matumizi salama na sahihi ya dawa, hatua inayolenga kulinda afya ya jamii na kuhakikisha usalama wa chakula kinachozalishwa nchini.




Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...