Na Seif Mangwangi, Michuzi TV Arusha
MKUTANO wa 153 wa Jumuiya ya Mabunge Duniani (IPU), unatarajiwa kufanyika nchini Tanzania huku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan akitarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa Mkutano huo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo 4 Agosti 2026, Jijini Arusha, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Azzan Zungu amesema mkutano huo utafanyika katika kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC) kuanzia Oktoba5 Hadi 9, 2026.
Amesema Tanzania iko tayari kupokea ujumbe wa wageni zaidi ya 2000 watakaohudhuria mkutano huo ikiwemo maspika wa Mabunge kutoka nchi 183 Duniani, Wabunge, Maafisa wa Bunge na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa na Kikanda, Wanadiplomasia, Washirika wa Maendeleo, Mashirika ya Kiraia, Taasisi za Elimu ya Juu pamoja na Vyombo vya Habari kutoka pande zote za dunia.
" Ni mkutano wa kihistoria kufanyika nchini kwetu na ni heshima kubwa sana tuliyopewa kama nchi, hivyo hi ni fursa adhimu sana ambayo inaonyesha namna dunia ina imani na nchi yetu katika kuendesha masuala ya utawala Bora," Amesema Spika Zungu.
Amesema masuala muhimu ya Kimataifa yatajadiliwa wakati wa Mkutano huo ikiwemo, Utawala wa Kidemokrasia, Amani na Usalama, Mabadiliko ya Tabianchi, Mabadiliko ya Kidijitali, Akili Unde, Ushiriki wa Walemavu, Vijana na Wanawake, Ustahimilivu wa Kiuchumi na Malengo ya Maendeleo Endelevu.
" Tuna imani kubwa kuwa, pamoja na mambo mengine, majadiliano hayo yatatoa mchango mkubwa katika kutatua changamoto zinazoikabili dunia kwa sasa ikiwa ni pamoja na Mabadiliko ya Tabianchi, Migogoro ya Kimataifa na Ugumu wa Maisha," Amesema na kuongeza:.
"Hii itadhihirisha kuwa Diplomasia ya Kibunge ina umuhimu mkubwa katika kutatua changamoto tunazokabiliana nazo kupitia majadiliano, makubaliano na ushirikiano kati ya Mataifa,".
Amesema mkutano huo pia utaimarisha ushirikiano wa Kimataifa, kukuza ushirikiano wa kimkakati na kutoa fursa adhimu kwa Sekta za Utalii, Usafirishaji na Huduma nchini Tanzania na zaidi, Mkutano huo utatoa fursa ya kuionesha dunia utajiri uliokuwepo nchini wa utamaduni, fursa za uwekezaji na vivutio vya utalii vinavyotambulika duniani.
Aidha Spika Zungu amesema katika mkutano huo, Rais wa Mabunge Duniani Dkt Tulia Ackson ambaye pia Spika mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, atastaafu nafasi hiyo baada ya kumaliza muda waje na kutoa fursa Kwa Spika mwingine kuchaguliwa.
"Ni jambo la kujivunia kuwa, Mtanzania mwenzetu, Mhe. Dkt. Tulia Ackson (Mb.) ndio Rais wa IPU kwa sasa, nafasi ambayo ameishika tangu Mwaka 2023 na kuitumikia vema katika kuhakikisha ufanikishaji wa Dira hiyo," amesema.
Inter-Parliamentary Union (IPU) ni Umoja wa Mabunge 183 Duniani ulioanzishwa Mwaka 1889.


.jpeg)
.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...