-Ni mashindano ya mbio za baiskeli za km 109 kutoka Dar hadi Bagamoyo
Katika hatua muhimu kwa maendeleo ya mchezo wa kuendesha baiskeli nchini Tanzania, Vodacom Tanzania Plc kwa kushirikiana na Chama cha Baiskeli Tanzania (CHABATA), leo imetangaza rasmi kubadilishwa kwa jina la msafara wa baiskeli wa Twende Butiama na kuwa Nyerere Cycling Tour, huku pia wakitangaza kuzindua mashindano mapya ya mbio za baiskeli za kilomita 109 za Vodacom Coastal Classic, zinazolenga kuiweka Tanzania kwenye ramani ya kimataifa ya mashindano ya baiskeli.
Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2016, msafara huu umekuwa ukienzi urithi wa kudumu wa Mwalimu Julius K. Nyerere kwa kuendeleza fursa sawa kwa wote kupitia uboreshaji wa mazingira ya kujifunzia, ujenzi wa miundombinu ya vyoo, pamoja na kuchangia vifaa vya kuwawezesha wanafunzi wenye mahitaji maalum ili kila mtoto aweze kupata fursa ya elimu.
Hadi sasa, msafara huo umefikia zaidi ya shule 107 na kuboresha maisha ya wanafunzi zaidi ya 75,000 wanaofaidika kupitia ujenzi wa madarasa bora na jumuishi yanayokidhi mahitaji ya wanafunzi wote.
Vodacom Tanzania Foundation ilianza kushirikiana na CHABATA kufadhili msafara huu miaka mine iliyopita, na katika kipindi hicho msafara wa Twende Butiama umekuwa mara nne zaidi, huku ukivutia washiriki kutoka Tanzania, ukanda wa Afrika Mashariki na kimataifa. Msafara wa mwaka huu utafanyika kuanzia tarehe 5 hadi 14 Oktoba 2026, washiriki wakianzia Bagamoyo hadi Butiama.
Ili kuakisi dhamira kuu ya msafara huu unaoenzi urithi wa Mwalimu Nyerere huku ndani yake wakipanga kuyawezesha kukua ili kuwa mashindano ya kimataifa ya baiskeli, kuanzia mwaka huu msafara huu utajulikana rasmi kama Nyerere Cycling Tour.
Dhamira ya mwaka huu ni moja: kukuza mchezo wa baiskeli na kuiweka Tanzania katika ramani ya kimataifa ya mchezo wa baiskeli. Kwa kushirikiana na CHABATA, Vodacom Tanzania inazindua mashindano makubwa ya baiskeli ya Vodacom Coastal Classic, yakihusisha mbio za kilomita 109 zitakazoshirikisha waendesha baiskeli wa kiume na wa kike.
Mbio hizi zitaanzia Dar es Salaam, kuelekea kaskazini hadi Makurunge mkoani Pwani na kumalizikia katika eneo la kihistoria la Old Boma, Bagamoyo, zikikamilisha safari ya kilomita 109. Kwa mara ya kwanza mashindano haya yatafanyika Jumapili, tarehe 4 Oktoba 2026, siku moja kabla ya kuanza kwa msafara wa baiskeli wa Nyerere Cycling Tour. Baada ya hapo, Vodacom Tanzania itaendesha mashindano haya kila mwaka ifikapo Jumapili ya kwanza ya mwezi Oktoba.
Kwa mara ya kwanza, washiriki zaidi ya 400 kutoka Tanzania na mataifa mbalimbali duniani wanatarajiwa kushiriki katika mbio hizi, "Tunataka kukuza mchezo huu," alisema Nguvu Kamando, Mkurugenzi wa Vodacom Business. "Kila siku tunaona waendesha baiskeli kwenye barabara zetu, aidha wakiwa ni wataalamu au washiriki wa kawaida. Hakuna sababu kwa nini Abella kutoka Mwanza asiweze kushindana hapa Tanzania na kwenye majukwaa ya kimataifa, au Saidi kutoka Shinyanga. Wanachohitaji ni vifaa sahihi na mafunzo sahihi. Vodacom Coastal Classic inalenga kuhamasisha na kuwapa motisha Watanzania wengi zaidi kuingia katika mchezo huu."
Gabriel Landa, Mwanzilishi wa Nyerere Cycling Tour, alisema, "Nyerere Cycling Tour imekuwa zaidi ya msafara wa baiskeli. Ni kuhusu kuendeleza maono ya Mwalimu Nyerere ya heshima na fursa sawa kwa kila Mtanzania. Kubadilisha jina la mashindano haya kwa heshima yake, sambamba na kuanzisha mbio za kiwango cha kimataifa za Vodacom Coastal Classic, ni mwanzo wa safari mpya. Tunajenga jukwaa ambalo vipaji vya Watanzania vinaweza kuibuka na kuvutia waendesha baiskeli kutoka kote duniani kuja kushiriki.
Tarehe Muhimu
- Vodacom Coastal Classic (Mashindano ya kilomita 109): Jumapili, 4 Oktoba 2026 — Dar es Salaam hadi Makurunge, zikimalizikia Old Boma, Bagamoyo.
- Nyerere Cycling Tour: Tarehe 5–14 Oktoba 2026 — Bagamoyo hadi Butiama.
Kuhusu Nyerere Cycling Tour
Awali ikijulikana kama msafara wa baiskeli wa Twende Butiama, Nyerere Cycling Tour inaenzi urithi wa Mwalimu Julius K. Nyerere kwa kuhamasisha uboreshaji na upatikanaji sawa wa elimu hapa nchini. Kupitia mashindano haya, zaidi ya shule 107 zimewezeshwa na zaidi ya wanafunzi 75,000 sasa wanafaidi mazingira bora na jumuishi ya kujifunzia.
Mkurugenzi wa Vodacom Business Nguvu Kamando, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu msimu mpya wa msafara wa Nyerere Cycling Tour (zamani Twende Butiama) utakaozinduliwa mnamo mwezi wa kumi ukiambatana na mashindano ya mbio za Vodacom Coastal Classic.
Wadau na Washiriki wa msafara wa mbio za Nyerere Cycling Tour (zamani Twende Butiama) wakipiga makofi kama ishara ya kufurahia ujio wa mashindano ya mbio za Vodacom Coastal Classic.
Mwanzilishi wa Msafara wa Mbio za Twende Butiama, Gabriel Landa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu msimu mpya wa msafara wa Nyerere Cycling Tour (zamani Twende Butiama) utakaozinduliwa mnamo mwezi wa kumi.
Wadau wa msafara wa Cycling tour (zamani Twende Butiama) wakisikiliza kwa makini kuhusu msimu mpya wa msafara huo na ujio wa Mashindano ya Vodacom Coastal Classic utakaozinduliwa mnamo mwezi wa kumi mwaka huu.



.jpeg)
.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...