Na Mwandishi Wetu, Dodoma
CHUO Kikuu cha Dodoma (UDOM), kupitia kampuni ya ubunifu ya MaxwellTrack Technologies, kimebuni mfumo wa kidijitali unaolenga kusaidia kampuni za bima kufuatilia mienendo ya magari na kupata taarifa sahihi za mazingira ya ajali ili kurahisisha utoaji wa fidia.

Mfumo huo unafuatilia mwenendo wa gari kabla na wakati wa ajali, ikiwemo kasi ya gari, eneo lilipotokea tukio, muda wa ajali pamoja na taarifa nyingine muhimu zinazoweza kusaidia kubaini chanzo na mazingira ya ajali.

Akizungumza katika Maonesho ya Kilimo ya Kimataifa Nane Nane yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Samwel Malecela, Nzuguni jijini Dodoma, Mhadhiri Msaidizi wa UDOM na Mwanzilishi wa MaxwellTrack Technologies, Jospeter Kaizilege, amesema ubunifu huo umejikita katika kutatua changamoto ya upatikanaji wa taarifa sahihi wakati wa kushughulikia madai ya fidia.

Amesema mara nyingi kampuni za bima hukumbana na changamoto ya kupata ushahidi wa kutosha kuhusu mazingira yaliyosababisha ajali, hali inayoweza kuchelewesha mchakato wa kufanya maamuzi kuhusu madai ya wateja.

“Changamoto kubwa imekuwa pale mteja anapopata ajali na kampuni ya bima kuhitaji uthibitisho wa mazingira yaliyosababisha ajali. Mfumo wetu unarekodi taarifa zote muhimu, hivyo unarahisisha kampuni ya bima kufanya maamuzi kwa kutumia ushahidi uliopo kwenye mfumo,” amesema Kaizilege.

Ameeleza kuwa mfumo huo umeundwa kwa kuzingatia mazingira ya Afrika, tofauti na baadhi ya vifaa vya GPS vinavyoagizwa kutoka nje ambavyo vinaweza kukumbana na changamoto za utendaji katika maeneo yenye mawasiliano hafifu.

Kwa mujibu wa Kaizilege, teknolojia hiyo inaweza kufanya kazi katika maeneo yenye changamoto za mawasiliano, hatua inayolenga kuhakikisha taarifa muhimu za gari na ajali zinapatikana kwa wakati unaohitajika.

Amesema matumizi ya mfumo huo yanaweza kusaidia kampuni za bima kupunguza migogoro inayohusiana na madai ya fidia, huku wateja wakinufaika na uwazi zaidi kutokana na kuwepo kwa taarifa za ajali zinazoweza kufikiwa kwa urahisi.

Kaizilege amesema wazo la ubunifu huo lilianza mwaka 2022 akiwa mwanafunzi wa UDOM, kama mradi wa mwisho wa masomo, kabla ya kuendelezwa kupitia programu za ubunifu za chuo hicho na hatimaye kuanzishwa rasmi kwa MaxwellTrack Technologies.

“Tumeanza rasmi kutoa huduma nchini Tanzania kwa takribani mwezi mmoja sasa na lengo letu ni kupanua huduma kwenda Kenya na Rwanda. Pia tunaendelea kushirikiana na mamlaka husika pamoja na kampuni mbalimbali za bima ili kuunganisha mfumo wetu na mifumo yao na kuhakikisha teknolojia hii inanufaisha sekta ya bima na usafirishaji kwa ujumla,” amesema Kaizilege.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...