Na Mwandishi Wetu, Dodoma
TAASISI ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imeongeza kasi ya utafiti wa kijiosayansi nchini kwa lengo la kuvutia uwekezaji katika sekta ya madini, kuongeza ajira, mapato ya Serikali na kuharakisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Akizungumza katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa GST, Mhandisi Ally Samaje, alisema taasisi hiyo ndiyo msingi wa mnyororo mzima wa sekta ya madini kwa kuwa hukusanya, kuchakata, kuhifadhi na kusambaza taarifa muhimu za kijiosayansi kwa wawekezaji na wadau mbalimbali.
Alisema GST imekamilisha utafiti wa jiolojia kwa asilimia 98 ya eneo lote la Tanzania, huku utafiti wa kijiofisikia wa kiwango cha kawaida ukifikia asilimia 100, hatua inayowapa wawekezaji taarifa za awali kuhusu maeneo yenye fursa za madini.
Kwa upande wa utafiti wa kijiofisikia wa kina (High Resolution Airborne Geophysical Survey), alisema taifa limefikia asilimia 16, huku maandalizi ya kuongeza kiwango hicho yakiendelea kupitia programu mpya za urushaji ndege katika maeneo yenye rasilimali nyingi za madini.
Mhandisi Samaje alifafanua kuwa awamu ya kwanza ya programu hiyo itahusisha utafiti katika eneo linalokadiriwa kuwa asilimia 18 ya ukubwa wa nchi, hatua itakayoongeza kiwango cha utafiti huo hadi asilimia 34 mara baada ya kukamilika. Aliongeza kuwa mkandarasi wa kazi hiyo tayari amepatikana.
Alisema awamu inayofuata itafanyika katika maeneo ya katikati ya Tanzania yenye ukubwa wa takribani asilimia 19 ya nchi, jambo litakalowezesha kufikia zaidi ya asilimia 50 ya utafiti wa kijiofisikia wa kina kabla ya mwaka 2030, kama ilivyoainishwa katika malengo ya Serikali.
Akizungumzia utafiti wa kijiokemia, alisema GST imefikia asilimia 24 ya eneo la nchi, huku ikipanga kufanya tafiti katika maeneo mapya 18 ndani ya mwaka huu wa fedha ili kuongeza kiwango hicho hadi asilimia 30.
Alieleza kuwa maeneo mengi yatakayofanyiwa utafiti yamechaguliwa kutokana na uwepo wa wachimbaji wadogo, ambao watanufaika na taarifa za kisayansi zitakazowasaidia kufanya uchimbaji kwa uhakika badala ya kubahatisha, kuongeza uzalishaji na kuboresha kipato chao.
Aidha, alisema taarifa hizo zitawawezesha wachimbaji wadogo kupata mikopo kutoka taasisi za fedha, huku GST ikiwa tayari kuthibitisha matokeo ya tafiti zake ili kuongeza imani ya wakopeshaji.
Mhandisi Samaje alibainisha kuwa utekelezaji wa programu hizo unawezeshwa na Mfuko wa Utafiti wa Madini unaotokana na fedha za retention zinazokusanywa kupitia sekta ya madini, ambazo zimeiwezesha GST kupanua shughuli zake za utafiti nchini.
Alisisitiza kuwa upatikanaji wa taarifa sahihi za kijiosayansi utapunguza hatari kwa wawekezaji, kuongeza uwekezaji katika utafiti na uchimbaji wa madini, kuchochea uanzishaji wa migodi mipya, kuimarisha viwanda vinavyotumia madini kama malighafi na kuongeza mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa taifa kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.



.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...