NA DENIS MLOWE - DAR ES SALAAM

VICTORIA Group (VG) imetangaza kuandaa mbio za afya za VG Fun Run zitakazofanyika Agosti 8, 2026 katika viwanja vya Victoria Park, Ununio jijini Dar es Salaam, zikiwa na lengo la kuhamasisha afya, kuimarisha mshikamano wa wanachama na kuwashirikisha wananchi katika mazoezi ya mwili.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Kamati ya VG Fun Run, Isidori Msaki, alisema wazo la kuanzisha mbio hizo limetokana na ukweli kuwa Victoria Group imekuwa pamoja kwa zaidi ya miaka 26 na sasa wanachama wengi wamefikisha umri wa zaidi ya miaka 50, jambo lililowasukuma kuweka kipaumbele kwenye afya zao.

Alisema Victoria Group ina wanachama 113 ambao pamoja na familia zao wanafikia takribani watu 700, hivyo wameona ni muhimu kuanzisha shughuli ya pamoja itakayowahamasisha kufanya mazoezi na kuishi maisha yenye afya.

Msaki alisema mbio hizo zitahusisha kukimbia umbali wa kilomita 10 kuanzia saa 12:00 asubuhi, huku washiriki wote watakaomaliza wakitunukiwa medali na kuandaliwa huduma ya supu, wakati wadhamini wa tukio watapatiwa vyeti vya shukrani kwa mchango wao.

Alisema tukio hilo halitawahusu wanachama wa Victoria Group pekee, bali pia limefunguliwa kwa marafiki na wananchi wote wanaotaka kushiriki.

Msaki alisema washiriki kutoka nje ya Victoria Group watatakiwa kulipa shilingi 30,000 ambazo zitajumuisha fulana maalumu, namba ya ushiriki pamoja na medali baada ya kumaliza mbio.

Aliongeza kuwa kwa wale wasioweza kushiriki mbio za kilomita 10, waandaaji wameandaa programu maalumu ya mazoezi ya aerobics itakayofanyika katika Victoria Park chini ya wakufunzi wa mazoezi, sambamba na burudani ya muziki na shughuli nyingine za kijamii.

Msaki alisema hadi sasa zaidi ya washiriki 126 wamekwishajisajili, huku matarajio yakiwa kufikisha zaidi ya washiriki 200 kabla ya siku ya tukio.

Naye Mwenyekiti wa Victoria Group, Sabasaba Mushingi, alisema kikundi hicho kilianzishwa takribani miaka 26 iliyopita kwa lengo la kujenga mshikamano na kusaidiana katika nyakati za furaha na huzuni, lakini kadiri miaka ilivyokwenda wamepanua shughuli zao hadi kwenye uwekezaji wa kiuchumi.

Alisema kwa sasa Victoria Group inamiliki vitega uchumi mbalimbali ikiwemo Victoria Park yenye thamani inayokadiriwa kuzidi shilingi bilioni moja kwa tathmini ya sasa, pamoja na uwekezaji katika hati fungani za Serikali na hisa.
Mushingi alisema VG Fund Run ni mwanzo wa safari ya kulifanya tukio hilo kuwa moja ya mbio kubwa nchini, zitakazokuwa zikifanyika kila mwaka na kuvutia washiriki wengi zaidi kutoka ndani na nje ya Victoria Group.

Alieleza kuwa baada ya tathmini ya tukio la mwaka huu, uongozi unapanga kuliboresha zaidi ili katika miaka ijayo liwe na zawadi kubwa, washiriki wengi zaidi na pia liwe jukwaa la kuchangisha fedha kwa ajili ya kusaidia jamii kupitia miradi mbalimbali ya kijamii.

Aliwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi Agosti 8 katika Victoria Park, Ununio, kushiriki siku ya mazoezi, afya na burudani, akisisitiza kuwa lengo kuu la Victoria Group ni kujenga jamii yenye afya bora huku ikiendeleza mshikamano na utamaduni wa kusaidiana.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...