Vodacom Tanzania PLC kupitia programu ya Classroom for Community Impact iliyo chini ya Vodacom Tanzania Foundation imekabidhi madarasa mawili yaliyokarabatiwa, madawati 30 pamoja na vifaa muhimu vya shule kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Ihowanja, wilayani Malinyi mkoani Morogoro, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika shule za msingi za umma.
Makabidhiano hayo yaliyofanyika jana yanalenga kuchangia uboreshaji wa miundombinu na mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi, hususan wenye mahitaji maalum.
Kupitia mpango huo, katika awamu hii Vodacom Tanzania imekarabati na kujenga jumla ya madarasa sita pamoja na kutoa madawati 90 katika shule tatu za msingi za umma za Vikindu, wilayani Mkuranga mkoani Pwani; Ihowanja, Malinyi mkoani Morogoro na Mahilo, wilayani Songea mkoani Ruvuma.
Katika Shule ya Msingi Ihowanja, msaada huo umehusisha ukarabati wa ujenzi wa madarasa mawili na utoaji wa madawati 30. Aidha, wanafunzi wamepatiwa mahitaji muhimu ya shule, ikiwemo madaftari, chupa za kubebea maji, kalamu na mabegi.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mkuu wa Kanda ya Kati wa Vodacom Tanzania PLC, Chiha Nchimbi, alisema mpango huo ni sehemu ya mchango wa kampuni katika kusaidia jamii na kuboresha mazingira ambayo watoto wanapata elimu.
Alisema uwepo wa madarasa salama, madawati ya kutosha na mazingira rafiki ya kujifunzia ni muhimu katika kuwawezesha wanafunzi hasa wenye mahitaji maalum, kushiriki kikamilifu katika masomo yao.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ihowanja, Iddy Mgonja aliishukuru Vodacom Tanzania kwa msaada huo, akisema utakuwa na mchango mkubwa katika kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia shuleni hapo, hasa kwa kupunguza changamoto ya upungufu wa madarasa na madawati.
Mgonja alisema ukarabati wa madarasa mawili pamoja na kupatiwa madawati 30 na vifaa muhimu vya shule kutawawezesha wanafunzi kupata mazingira salama na rafiki zaidi ya kujifunzia, huku walimu wakipata mazingira bora ya kutekeleza majukumu yao ya kufundisha.
Kwa upande wa serikali na uongozi wa jamii, makabidhiano hayo yalishuhudiwa na Diwani wa Kata ya Kilosampepo, Boniventure Killian Mwanga, pamoja na Mwenyekiti wa Kijiji cha Ihowanja, Mohamed Fidelis Kilamala pamoja na viongozi na wadau wengine wa elimu.
Viongozi hao wamepongeza uwekezaji huo wakisema utasaidia kupunguza changamoto za miundombinu ya elimu na kuweka mazingira bora na salama zaidi kwa wanafunzi na walimu. Wamesisitiza kuwa ushirikiano kati ya sekta binafsi, serikali na jamii ni muhimu katika kuharakisha upatikanaji wa miundombinu bora na jumuishi ya elimu, hususan kwa watoto wenye mahitaji maalum.
Mpango wa Classroom for Community Impact ni sehemu ya jitihada za Vodacom Tanzania kupitia Vodacom Foundation za kushirikiana na jamii katika kuboresha mazingira ya elimu na kusaidia kujenga mazingira jumuishi zaidi ya kufundishia na kujifunzia kwa watoto nchini.
Mkuu wa Kanda ya Kati wa Vodacom Tanzania PLC, Chiha Nchimbi (kulia), akikabidhi dawati kwa Diwani wa Kata ya Kilosampepo, Boniventure Killian Mwanga (kushoto), dawati hilo ni mojawapo ya madawati 30 yaliyokabidhiwa katika Shule ya Msingi Ihowanja, Malinyi mkoani Morogoro, kupitia mpango wa Classroom for impact ulioko chini ya Vodacom Tanzania Foundation. Kupitia mpango huo, Vodacom Tanzania imekarabati na kujenga madarasa sita pamoja na kutoa madawati 90 katika shule tatu za msingi za umma za Vikindu (Mkuranga - Pwani), Ihowanja (Malinyi - Morogoro) na Mahilo (Ruvuma) kwa lengo la kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia, hususan kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum. Hafla hiyo ilifanyika mwishoni mwa wiki katika Shule ya Msingi Ihowanja, wilayani Malinyi mkoani Morogoro. Wengine katika picha ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ihowanja, Iddy Mgonja (wa pili kushoto), na Mwenyekiti wa Kijiji cha Ihowanja, Sylvester Mgwasa.
Wafanyakazi wa Vodacom Tanzania PLC wakitayarisha mahitaji ya shule, ikiwemo madaftari, mabegi na kalamu kwa ajili ya kutoa msaada kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Ihowanja, Malinyi-mkoani Morogoro wakati wa hafla ya makabidhiano ya madarasa mawili na madawati 30 yaliyofanyika shuleni hapo kupitia Vodacom Tanzania Foundation. Msaada huo unalenga kuwapa wanafunzi vifaa muhimu vya kujisomea, ikiwa ni sehemu ya dhamira ya kampuni hiyo kuhakikisha mazingira bora ya kujifunzia yanaenda sambamba na upatikanaji wa vifaa vya elimu kwa watoto.
Baadhi ya vikapu vyenye mahitaji muhimu ya shule kwa ajili ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Ihowanja, iliyoko wilaya ya Malinyi, mkoani Morogoro, vikiwemo madaftari, chupa ya maji, kalamu, soksi na mabegi, vikiwa tayari kwa ajili ya kugawiwa kwa wanafunzi. Vifaa hivyo vilitolewa na Vodacom Tanzania PLC sambamba na makabidhiano ya madarasa mawili na madawati 30 yaliyofanyika shuleni hapo, chini ya mpango wa kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia, hususan kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Baadhi ya Wanafunzi wa Shule ya Msingi Ihowanja, Malinyi-mkoani Morogoro, wakiwa katika baadhi ya madawati yaliyotolewa na Vodacom Tanzania Foundation ndani ya moja ya madarasa yaliyokarabatiwa kupitia mpango unaolenga kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa wanafunzi. Kupitia mpango huo, Vodacom Tanzania Plc imekarabati na kujenga madarasa sita pamoja na kutoa madawati 90 katika shule tatu za msingi za umma za Vikindu (Pwani), Ihowanja (Morogoro) na Mahilo (Ruvuma).



.jpeg)
.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...