Na Mwandishi Wetu
MKURUGENZI wa Sera na Mipango, Needpeace Wambuya, amevitaka Vyama vya Ushirika nchini kutumia teknolojia ya kisasa katika uzalishaji na uongezaji thamani wa bidhaa ili ziweze kukidhi viwango na mahitaji ya masoko ya ndani na nje ya nchi.

Wambuya ameyasema hayo katika Maonesho ya Kimataifa yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Samwel Malecela jijini Dodoma, alipokuwa akimwakilisha Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga.

Amesema Vyama vya Ushirika ni nguzo muhimu katika kukuza uchumi wa nchi kwa kuwa vinawakusanya wananchi pamoja, hususan wakulima na wafugaji, na kuwawezesha kushirikiana katika uzalishaji, utafutaji wa masoko na upatikanaji wa mitaji.

Wambuya amesema ameridhishwa na namna Vyama vya Ushirika vilivyojipanga katika kuunganisha nguvu za wanachama, kuongeza uzalishaji na kutafuta masoko ya uhakika kwa bidhaa zao, hatua ambayo alisema inasaidia kuongeza tija na kipato kwa wanachama.

“Vyama vya Ushirika vinapaswa kutumia teknolojia ya sasa ili kuongeza uzalishaji na kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa zinakuwa na ubora unaokidhi viwango vya masoko ya ndani na nje ya nchi,” amesema Wambuya.

Aidha, Wambuya amesema zao la kakao linalozalishwa mkoani Mbeya ni miongoni mwa mazao yenye ubora na kuwataka wazalishaji pamoja na Vyama vya Ushirika kuhakikisha bidhaa hiyo inawekewa nembo ya Tanzania ili kuongeza utambulisho wake na ushindani katika masoko ya kimataifa.

Amesema matumizi ya teknolojia, ubunifu na uongezaji thamani wa mazao ni muhimu katika kuwawezesha wakulima kupata tija zaidi, kuongeza thamani ya bidhaa na kuchangia kwa kiwango kikubwa katika maendeleo ya uchumi wa nchi.

Wakati huohuo, Wambuya amewataka Vyama vya Ushirika kuendelea kuimarisha mifumo ya uzalishaji na uongezaji thamani wa mazao ya kahawa na pamba ili kuhakikisha wakulima wanaendelea kunufaika na rasilimali hizo na kupata masoko yenye tija.

Amesema hatua hiyo itawezesha mazao hayo kuwa na ushindani zaidi katika masoko ya ndani na kimataifa, huku ikiongeza kipato cha wakulima na kuimarisha mchango wa sekta ya ushirika katika uchumi wa Taifa.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...