Na Belinda Joseph – Dodoma.

CHAMA Kikuu cha Ushirika wa Mazao Songea na Namtumbo (SONAMCU) mkoani Ruvuma kimesema mfumo wa Stakabadhi za Ghala umeendelea kuwanufaisha wakulima wake, huku kikijivunia kuwalipa wanachama kwa wakati bila kuwepo malalamiko yoyote.

Akizungumza na waandishi wa habari Agosti 3, 2026, katika Maonesho ya Kilimo Nanenane Kitaifa yanayoendelea jijini Dodoma, Mwenyekiti wa SONAMCU, Ally Hassan Chemka, amesema chama hicho kinaendelea kufanya vizuri katika usimamizi wa mazao kupitia mfumo wa Stakabadhi za Ghala, hali iliyochangia kuongeza imani ya wakulima na kuimarisha huduma kwa wanachama.

Chemka amesema sambamba na mafanikio hayo, SONAMCU inaendelea na ujenzi wa ofisi yake mpya katika mtaa wa Mahenge, Songea Mjini, ambapo ujenzi huo umefikia hatua za mwisho kukamilika, amesema ifikapo Oktoba mwaka huu, chama hicho kitaanza pia ujenzi wa ofisi ya tawi la SONAMCU Wilaya ya Namtumbo.

Ameeleza kuwa tayari chama kimejenga maghala mawili pamoja na nyumba ndogo ya watumishi, huku katika mwaka wa fedha 2026/2027 kikitarajia kujenga ofisi yenye ukumbi wa mikutano na maghala manne ya kuhifadhia mazao ili kuongeza uwezo wa kuhudumia wanachama.

Aidha amesema SONAMCU imejipanga kununua malori manne yatakayotumika kusafirisha pembejeo na mazao ya wanachama kwenda kwenye maghala ya kuhifadhia, pamoja na kununua gari la kisasa la chama litakalorahisisha shughuli za usafiri na uratibu wa mikutano katika mikoa yote inayohudumiwa na chama hicho.

Akizungumzia ushiriki wao katika Maonesho ya Nanenane, Chemka amesema maonesho hayo ni muhimu kwa kuwa yanawakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo, hivyo yamewapa fursa ya kujifunza mbinu mpya za uzalishaji wa mbegu bora, kupata uzoefu kutoka kwa vyama vingine vya ushirika na kutambua masoko mapya ya mazao.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa SONAMCU, Hajji H. Haule, amesema chama hicho kinawahudumia wakulima wa mazao ya tumbaku, mbaazi na ufuta, huku uzalishaji katika mwaka wa fedha 2025/2026 uzalishaji wa tumbaku uliongezeka kutoka tani 1,800 hadi tani 2,800, wakati uzalishaji wa mbaazi uliongezeka kutoka tani 4,000 hadi tani 11,000.

Amesema uzalishaji wa ufuta haukuwa mkubwa katika msimu uliopita kutokana na changamoto ya mvua na kwa msimu wa mwaka 2026/2027, SONAMCU imejipanga kuongeza uzalishaji wa mazao yote inayoyasimamia kupitia kuendelea kuwawezesha wakulima na kuboresha huduma zinazotolewa na chama hicho.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...